Sunday, February 12, 2017

MASAA 72 YA ASKOFU GWAJIMA MAHABUSU YA POLISI

Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati sakata la kutangaza na kushikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam watu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.



Pia alieleza kushangazwa kwake na baadhi ya wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa nchini kuingizwa katika sakata hilo hata kabla uchunguzi kufanyika.



Gwajima ambaye alikuwa ameshikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam alikokwenda baada ya kutangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya, alisema hana mpango wa kumshtaki mkuu huyo wa mkoa.



Askofu Gwajima alisema badala yake anakata rufaa kwa Rais Magufuli akimtaka kufuatilia tuhuma hizo kwa undani kwa watu wanaoendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi ili waweze kupata haki.



Akizungumza kanisani kwake Dar es Salaam jana, Gwajima alisema alishikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kwenda kuitikia mwito uliotolewa na Makonda kwa ajili ya kutoa ushirikiano kuhusu tuhuma za dawa za kulevya



Alisema baada ya kufika kituoni hapo na kufanyiwa mahojiano alikutana na mfanyabishara na Diwani wa Mbagala Kuu, Yusuph Manji ambaye naye alikuwa amefika kituoni hapo kwa ajili ya kuitika mwito huo wa Makonda.



"Kwenye chumba changu tulikuwa mimi na Yusuph Manji, huyu ana kampuni zaidi ya 23 ameajiri Watanzania zaidi ya 5,000, sasa mtu kama huyo imeshindikanaje kumuita kwa kumpelekea hati ya kuitwa kuhojiwa, badala yake anatangazwa?"



"Imeshindikanaje mtu kama Manji kumuita kwa kumuandikia barua ili aende ahojiwe na ikigundulika achukuliwe hatua, kwa nini atangazwe kabla ya kuchukuliwa hatua?  Ilipaswa aandikiwe barua ya wito kisha uchunguzi ufanyike na kama akibainika ndiyo achukuliwe hatua, ila kwa sababu mkuu wa mkoa hakuwa na nia nzuri hata kwa Manji ndiyo maana hakufanya hivyo," alisema Gwajima.



Alisema hadi alipoachiwa katika kituo hicho bado Manji alikuwa ameshikiliwa na Jeshi la Polisi, ambapo alihoji sababu ya Manji na wengine wanaoendelea kushikiliwa kituoni hapo kutofanyiwa uchunguzi na ukaguzi kama aliofanyiwa yeye ili waachiwe kama yeye au kuchukuliwa hatua kama wakibainika kujihusisha na biashara hiyo.



"Sioni sababu ya kuendelea kuwashikilia watu wale bila kuchukuliwa hatua. Kama mimi nilituhumiwa tena kwa kutangazwa lakini mwishowe ikabainika hakuna ukweli, nitaamini vipi kama wale waliobaki ndani mikononi mwa Polisi nao wanahusika?"Alihoji Gwajima.



Gwajima alisema mbali na Manji na wafanyabishara wengine waliotajwa kuhusika na biashara hiyo, wamo pia askari wa Polisi ambao nao wanatuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo na wameendelea kushikiliwa kwa amri ya mkuu wa mkoa.



Kutokana na hali hiyo, Gwajima alisema ameamua kukata rufaa kwa Rais ili aweze kuwaangalia watu hao kwa jicho la tatu na tuhuma dhidi yao ziweze kuchunguzwa na ukweli ujulikane.



"Mheshimiwa Rais ninakuomba sana, kuna wale watu wengine ambao nilikuwa nao, ambao ni wafanyabishara na walitangazwa kama mimi, naomba uwatazame kwa macho ya huruma ili tuhuma zao zishughulikiwe, kuliko kuendelea kukaa kwenye giza chini mule, kwa niaba yao ninakata rufaa kwako naomba uwahurumie.



"Kuna askari Polisi wapo ndani kwa wiki ya pili sasa kwa amri ya Makonda, mimi naomba niwasemee leo, kama mimi imeonekana kuwa sina makosa, vipi kuhusu wao? Nampongeza mheshimiwa Rais kwa kuingia katika vita ya dawa za kulevya naomba atazame jambo hili, "alisisitiza Askofu Gwajima.



Alisema kuwa alichogundua ni kuwa Rais anahitaji msaada wake hivyo anaingia katika kazi ya kumsaidia Rais kwa maelezo kuwa inawezekana anapata taarifa zisizo za ukweli.



Gwajima alisema kuwa leo amepanga kwenda Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuwaona watuhumiwa wengine ambao wanaendelea kushikiliwa.



Aeleza alivyokaguliwa

Katika hatua nyingine, Gwajima alisimulia waumini wa kanisa lake namna shughuli ya ukaguzi dhidi yake ilivyoendeshwa na Jeshi la Polisi, huku akidai amechiwa baada ya kubainika tuhuma dhidi yake hazikuwa na ukweli.



Alisema baada ya kuhojiwa alielezwa anatakiwa kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kufanyiwa vipimo ili kubaini kama anajihusisha na  utumiaji wa dawa za kulevya ama la, ikiwa ni pamoja na kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake ambapo alieleza kuwa licha ya kufanyiwa yote hayo Polisi walifikia pia hatua ya kukagua akaunti zake za fedha.



"Kwa sababu mimi tangu kuzaliwa sijawahi kuonja mambo hayo, lakini walivyopima wakakuta hamna chochote na wakanipa fomu kuonesha hawajakuta kitu.



"Niliwaambia kwangu mkikuta hata kipisi cha sigara andikeni dawa za kulevya, tulifika kwangu nyumba yangu ina ghorofa tatu wakakagua zote na hawakukuta kitu walichotaka," alisema



Aliongeza kuwa,"wakaona haitoshi, wakahamia kwenye akaunti zangu za benki na mimi nikawaruhusu waendelee walipofanya uchunguzi wao wakabaini hakuna kitu cha kuweza kunikamatia, hawakupata kitu wakaamua kuniachia,". 



Gwajima alisema hana mpango wa kumshtaki Makonda ama kumfungulia kesi bali anajua cha kumfanya.

No comments:

Post a Comment