Chama
cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), kimesema kipo kwenye maandalizi
ya kumkabidhi kadi mrembo wa Tanzania mwaka 2006, Wema sepetu, pamoja na
kundi lake lenye zaidi ya watu 500.
Wema
alikuwa mmoja kati ya wanachama maarufu wa CCM katika kundi la wasanii
wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka juzi kwa
kaulimbiu ya ‘mama ongea na mwanao’.
Akiwa kama kiongozi wa wasanii, alishiriki kumnadi Mgombea Mwenza wa CCM ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Katika
mkutano wake na wanahabari mwishoni mwa wiki, Wema alisema kwa sasa
ameamua kuvaa magwanda na yupo tayari kwa mapambano.
Mkuu
wa Idara ya Habari wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema),
Tumaini Makene jana alisema wapo kwenye maandalizi na kabla ya Machi
5, mwaka huu watamkabidhi Wema kadi ya uanachama na kundi lake
linalomuunga mkono.
“Wema atakabidhiwa kadi kwa utaratibu maalumu maana ameonyesha heshima na nia ya kujiunga kwenye mapambano ya kweli.
“Kwa kweli Chadema tunafarijika sana na kuja kwake maana kuna timu kubwa inayomuunga mkono pia wanataka kujiunga na chama.
“Tena
na wengine wanatoka katika mashirikisho mbalimbali ikiwamo TFF. Kwa
hiyo hapo unapata picha ya Wema ni mwanachama mpya wa Chadema mwenye
mvuto wa aina yake na huwezi kubeza hata kidogo kuja kwake,” alisema Makene
Alisema
wakati wowote chama hicho kitatangaza lini mwanachama huyo atakabidhiwa
kadi ya Chadema, tukio ambalo alisema litakuwa la aina yake.
Akizungumza
nyumbani kwao Sinza, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Wema alisema
amechukua uamuzi wa kuhama CCM baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda, kumtaja katika orodha ya watu wanaotumia dawa za kulevya.
Alisema kitendo hicho kilimdhalilisha kwa kiwango kikubwa.
No comments:
Post a Comment