Tuesday, February 21, 2017

MADIWANI CCM WASUSIA KIKAO NI BAADA YA KUKOSA IMANI NA MEYA

MADIWANI wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Manispaa ya Dodoma, jana walisusa kikao wakitaka Meya wa Manispaa hiyo, Jafari Mwanyemba kutokiendesha baada ya kukosa imani naye.

Meya huyo anadaiwa kutaka kufanya ubadhirifu wa Sh milioni 30 za mradi wa maji wa Zuzu.

Madiwani hao walikutana katika ukumbi wa manispaa hiyo ikiwa ni kikao chao kwa mujibu wa kanuni kabla ya kufanyika baraza la madiwani.

Akizungumza na waandishi wa habari  baada ya kutoka nje ya ukumbi huo, Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Jumanne Ngede alisema walifikia uamuzi huo baada ya Meya  kung’ang’ania kuendesha kikao licha ya wajumbe  kumtaka  asikiendeshe na badala yake amuachie katibu wa madiwani hao ndiyo akiongoze.

“Tupo nje ya kikao cha chama kwa sababu awali kabla ya kikao hicho Februari 13, mwaka huu madiwani tulijiorodhesha majina na kusaini madiwani 43.

“Tuliwasilisha hoja yetu kwa Mkurugenzi wa Manispaa kwa vile tuna shaka na Meya wetu,”alisema Naibu Meya.

Ngede ambaye ni Diwani wa Kata ya Chamwino alisema  walifuata kanuni zinazowataka   wanapokuwa na shaka wawe huru kuhoji na kuuliza.

“Tuliwasilisha hoja tano ambazo tulimtuhumu Meya kwa matumizi mabaya ya madaraka yake, matumizi mabaya ya fedha za mradi wa Zuzu.

“Tulianisha kila kitu kwa hatua na alitakiwa kujibu ndani ya siku tano na jana (juzi) alikabidhiwa barua ya tuhuma hizo,”alisema Ngede.

Hata hivyo alisema wakati wakiendelea na hatua hizo madiwani waliitwa na Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM usiku kwa nyakati tofauti, jambo ambalo liliwalazimu kutoa taarifa kwa Katibu wa CCM mkoa ambaye naye aliwajibu wasubiri uamuzi wa CCM wilaya.

“Sisi ambao tumejiorodhesha ndiyo tuliitwa kwenye kamati ya maadili, tukaona ili tusipotezwe nguvu za jambo hili tulienda kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM,  Philip Mangula.

“Tulimueleza  na kwa nia nzuri, mzee alisema ameyapokea sisi twende hivyo tuhuma za kuitwa kamati ya maadili zikasimamishwa,”alisema Ngede

  Diwani wa Kata ya Ipagala, Gombo Dotto, alisema madiwani wamefikia hatua hiyo kupaza sauti zao za kupinga ubadhirifu ndani ya manispaa hiyo.

“Kuna kundi la madiwani wanaojiita wao ndiyo wenye halmashauri na lipo kundi la waathirika ambao ndiyo la wengi hawajui halmashauri kunafanyika nini.  Yapo mengi ukiwamo wizi wa fedha na kikafikia hatua madiwani wahoji,”alisema Dotto.

“Aliomba ufadhili kutoka ubalozi wa Japan ambako mchakato uliendelea na mwaka 2015/16 ulitoa Sh milioni 122 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji Zuzu. Machi  mwaka jana fedha hizo zilipelekwa Manispaa kwa ajili ya mradi huo,”alisema Diwani huyo.

Alisema wakati wa kumpitisha mkandarasi ilikuwapo tenda ya kampuni moja kinyume na utaratibu na pia Aprili 13  mwaka jana Meya  alisaini mkataba na Aprili 20   fedha ikatolewa.

  Novemba mwaka jana Japan walitaka kufika kwenye mradi huo ambao walikuwa wakitumiwa picha lakini walipofika kwenye eneo la mradi walikuta hakuna kitu kilichofanyika na Sh  milioni 30 za awali zimeliwa.

“Japan walitaka fedha zirudishwe na Mkurugenzi wa Manispaa naye alitaka fedha hizo zirudishwe.  Desemba 20, mwaka huu Meya alirudisha fedha hizo kwa jina la Mdegela Investment ambayo ni kampuni yake na tena alisema anajitolea,” alisema diwani huyo.

“Mkurugenzi Godwin Kunambi alisema kwa kuwa kuna tuhuma za ubadhirifu na aliyelipwa ni mkandarasi, akaamua kumkamata mkandarasi (Kalago Enterprises Ltd) na kumpeleka polisi na alipobanwa aliwataja washirika wake akiwamo Meya huku akidai hakuonyeshwa hata sehemu ya kufanyia kazi,”alisema.

  Gombo alisema madiwani walifikia hatua hiyo ya kuhoji na  Meya akataka kuficha jambo hilo katika kikao cha bajeti cha Januari 26, mwaka huu.

Alisema  madiwani walitaka wajadili migogoro yao ndani ya chama na katika kujadili Meya aliamua kueleza halisi ya mradi na kuwaambia ameamua kujitolea kuilipa halmashauri Sh  milioni 30.

‘’Ni  kweli kama huhusiki unatoaje Sh milioni 30 za nyumbani kwako kuisaidia halmashauri wakati wewe hukupewa fedha hizo,”alisema .

 Mkurugenzi   Kunambi  alikiri kupokea hoja za madiwani hao zikiwa zimesainiwa na madiwani 43 kati ya 55.

 MTANZANIA ilimtafuta Meya Mwanyemba lakini alisema alikuwa  kikaoni.

No comments:

Post a Comment