KOCHA
wa Yanga, Mzambia George Lwandamina amesema kwamba mechi mbili dhidi ya
Ngaya Club ya Comoro zitawapa picha nzuri ya timu yao kabla ya kuvaana
na Simba Februari 25, mwaka huu.
Yanga
watamenyana na mahasimu wa jadi, Simba SC Februari 25, mwaka huu Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara.
Na
akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online juzi, Lwandamina alisema
kwamba mapema mno kuizungumzia mechi na Simba, kwa sababu kwanza wana
mechi za Ligi ya Mabingwa.
“Kwanza
tuna mechi na Wacomoro, tutacheza nyumbani na ugenini, mechi ambazo
zitatupa picha nzuri kabla ya kucheza na Simba,”alisema.
Yanga
watakuwa wageni wa Ngaya FC Jumapili mjini Ngaya kabla ya kurudiana
wiki inayofuata Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na baada ya hapo
watakwenda mafichoni kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba, Februari 25.
Mbio za ubingwa wa Ligi Kuu zimeshika kasi kwa sasa, miamba miwili ya soka nchini Simba na Yanga ikifukuzana kileleni.
Kwa
sasa, Yanga SC wapo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zao 49,
wakifuatiwa na Simba SC yenye pointi 48 lakini baada ya timu zote
kucheza mechi 21.
Na
hiyo ni baada ya matokeo mazuri kwa timun zote mwishoni mwa wiki, Yanga
wakianza kuiadhibu Stand United kwa mabao 4-0 Uwanja wa Taifa, Ijumaa
na Simba wakafuatia kwa kuitandika Maji Maji 3-0 Uwanja wa Maji Maji
Songea Jumamosi.
Wakati
mabao ya Yanga Ijumaa yalifungwa na Donald Ngoma, Simon Msuva, Obrey
Chirwa na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, ya Simba SC Jumamosi
yalifungwa na Ibrahim Hajib, Said Ndemla na Laudit Mavugo.
Mara
ya mwisho timu hizo zilikutana katika Nusu Fainali ya Kombe la
Mapinduzi Januari 10, mwaka huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar na Simba
ikashinda kwa penalty 4-2 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
Awali
ya hapo, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Oktoba 1,
mwaka huu na kutoka sare ya 1-1, Yanga wakitangulia kwa bao la Amissi
Tambwe kipindi cha kwanza kabla ya Simba kusawazisha kwa bao la Shizza
Kichuya kipindi cha pili.
No comments:
Post a Comment