KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Iddi Nassor Cheche amesema kwamba ushindi wa jana wa 1-0 dhidi ya Ndanda FC umekuwa mwendelezo mzuri wa wimbi lao la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na sasa wanazikazia mwendo Yanga na Simba kileleni.
Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online juzi, Cheche alisema kwamba ushindi huo unaofuatia ushindi wa 1-0 pia dhidi ya Simba ni chachu kwao kushinda mechi zijazo pia.
“Nimeupokea kwa furaha ushindi huu, nawapongeza sana wachezaji wangu kwa kazi nzuri waliofanya leo, hususan mfungaji wa bao (Yahya Mohammed),”alisema.
“Bado tuna kazi kubwa, tuna kazi kubwa sababu tunazidiwa pointi nyingi na timu zilizo mbele yetu, Yanga na Simba, kwa hiyo tunatakiwa kuendeleza wimbi la ushindi ili tuwafikie kama na wao watateleza huko mbele ya safari,”alisema.
Baada ya kuipiga Ndanda bao 1-0 juzi usiku Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Azam FC inafikisha pointi 37 baada ya kucheza mechi 21 na inaendelea kushika nafasi ya tatu.
Iko nyuma ya Yanga ambayo inayongoza kwa pointi zake 49, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 48 baada ya timu zote kucheza mechi 21 pia.
No comments:
Post a Comment