Monday, February 27, 2017

DC AAMUA KUBADILISHA MATUMIZI YA TSHS MIL.130

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ameagiza watendaji wa manispaa hiyo kuhamisha zaidi ya Sh milioni 130 zilizotengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya soko la Mkunguni ambalo uboreshaji huo umeshindwa kufanyika.

Badala yake ametaka fedha hizo zipelekwe katika soko la Maandazi ili kufanya uboreshaji wa miundombinu, ikiwemo ujenzi wa choo kipya. Hapi alitoa agizo hilo jana baada ya Ofisa Mtendaji wa kata ya Hananasif, Salum Zaganya kueleza mgogoro uliopo juu ya soko hilo la Mkunguni unakwamisha maendeleo ya kata yake.

"Inasikitisha kuona fedha zimekaa benki kwa miaka mitatu hazijafanya kazi, maana yake mmewacheleweshea wananchi maendeleo kwa miaka mitatu, hizo fedha zihamishwe haraka," alisema Hapi.

Mtendaji huyo wa kata alisema, mgogoro uliopo katika soko hilo ni baina ya wananchi wanaodai kumiliki viwanja wanaomiliki ndani ya soko hilo, wanaushirika wanaodai kuwa ni eneo lao na manispaa.

Mgogoro mwingine ni nyumba mbili zilizojengwa ndani ya manispaa hiyo.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema Sh milioni 37 zilitengwa katika mwaka wa fedha 2014/15 na mwaka wa fedha 2016/17 zikatengwa fedha nyingine Sh milioni 95. Alitaka fedha hizo zihamishwe haraka kwa kuwa zinavyozidi kukaa benki zinapungua.

Akifafanua suala hilo, mwakilishi wa Mchumi wa Manispaa hiyo, Febronia Luyagaza alisema, tathmini hufanyika kila mwisho wa mwaka na walishindwa kufanya kwa kuwa hawakupata maombi ya kuhamisha fedha hizo kutoka katika kata hiyo.

Katika hatua nyingine, Hapi aliagiza manispaa kuandika barua kwenda Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa ajili ya tathmini na kuiomba kuhamisha fedha hizo kwenda eneo lingine kwa ajili ya maendeleo.

Baada ya kutoa maagizo hayo Hapi alitembelea eneo linalodaiwa kuwa na mgogoro ambapo aliagiza kuundwa kwa kamati itakayowashirikisha wananchi, wanaushirika na manispaa ili kuona mnamna ya kumaliza mgogoro huo.

"Kaeni chini kupitia hiyo kamati ya pamoja ili muweke mambo yenu sawa kusudi serikali iweze kuleta pesa za maendeleo hapa," alisema.

No comments:

Post a Comment