Ezekieli Oluchi, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho amesema kitendo kilichofanywa na Hashium Mgandilwa, Mkuu wa wilaya ya Kigamboni kuagiza wakuu wa shule Kidete na Somangira kuvuliwa madaraka baada ya shule zao kushika mkia katika matokeo ya kidato cha nne ni kinyume cha sheria na anawashauri waalimu waandike malalamiko ili wamfikishe mahakamani.
“Mamlaka ya nidhamu kwa waalimu ni tume ya utumishi wa waalimu sio mkuu wilaya, tumewasiliana na Katibu wa chama cha waalimu mkoa wa Dar es Salaam ili wahusika waandikiwe barua wafuate sheria” alisema Oluochi.
Aliongeza “wahusika waliowashusha vyeo waalimu wakikataa kufuata sheria, waalimu husika wanapaswa kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, nakala kwa chama cha waalimu ili sisi tuweze kumfikisha mhusika mahakamani, kama waalimu husika hawataandika barua za malalamiko hatuwezi kumfikisha mkuu wa wilaya mahakamani.
Februari 1 mwaka huu Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni alitoa tamko kufuatia shule sita za Dar es Salaam kuwa miongoni mwa shule kumi za mwisho katika matokeo ya kidato cha nne na aliagiza wakuu wa shule mbili zilizopo kwenye manispaa hiyo za Kidete na Somangira kuchukuliwa adhabu kali ikiwemo kuvuliwa madaraka.
Mkuu huyo alisema hayo baada ya kuzitembelea shule hizo mbili na kufanya mazungumzo na wadau wa elimu wilayani humo.
Alinukuliwa akisema “nini tufanye kwa hali hii, nilivyofanya kikao cha mimi pamoja na wakuu wa shule tulikubaliana kwamba kwa mkuu wa shule yeyote atakayefelisha kupitiliza tutamvua madaraka na atabaki hapa hapa,”
Aliongeza, “Najua kuna viongozi wako hapa waliangalie hilo, hatuwezi kuendelea kulifurahia hilo wakati shule imekuwa ya mwisho kitaifa,”
Hata hivyo mkuu huyo wa shule ya Kidete alidai shule yake haikuwa ya mwisho kitaifa bali ilikuwa kwenye orodha ya shule ya shule kumi za mwisho kitaifa.
Akizungumzia suala la shule kuwa ya mwisho Oluochi, anasema ‘tusihangaike shule ipi imekuwa ya mwisho, maana hata wakipangwa waliopata daraja la kwanza, nako wa mwisho yupo, tuangalie ufaulu kwa ujumla na sababu za kushuka ufaulu kwa shule za serikali sababu zipo wazi”.
No comments:
Post a Comment