Monday, August 27, 2018

VYOMBO VYA HABARI VINA HAKI YA KUIKOSOA SERIKALI

MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, DK. HASSAN ABBAS.

MSEMAJI Mkuu wa serikali, Dk. Hassan Abbas, amesema vyombo vya habari vina haki ya kuieleza na kuikosoa serikali, sekta binafsi na jamii wanapokosea katika utekelezaji wa majukumu yao mbalimbali.

Aidha, amesema vyombo vya habari visivyofanya hivyo vitakuwa haviitendei haki jamii ambayo inawategemea.

Dk. Abbas ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa sherehe ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari za Jinsia, zilizoandaliwa na Umoja wa Mataifa, linaloshughulikia wanawake (UN Women) kwa kushirikiana na Gender Links.

Tuzo hizo zilitanguliwa na mkutano wa siku mbili wa kujadili masuala mbalimbali ya jinsia, hasa wajibu wa waandishi wa habari na umuhimu wa kuwa na wanahabari wengi ambao ni viongozi kwenye vyombo vya habari, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika nchini.

“Vyombo vya habari vina wajibu mpana katika masuala ya maendeleo, ya jinsia au maendeleo kwa upana wake…vina haki ya kutueleza sisi serikali na sekta binafsi wapi tunakosea kwenye sera, mipango na mikakati yetu ili hatua ziweze kuchukuliwa, wasipotekeleza watakuwa hawajaitendea haki jamii,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Abbas, vyombo vya habari ni muhimili wanne ambao unapaswa kutekeleza wajibu huo kwa kuangalia kama serikali na jamii kwa ujumla wanazingatia masuala ya jinsia na usawa wa wanawake.

“Vyombo vya habari ni wabia, wasibakie kuwa viranja na kutazama tu, pale wanapopaswa kuingia uwanjani na kucheza, basi huo ni wajibu wao pia wanakaribishwa,” alisisitiza.

Alisema vyombo hivyo visibaki kwenye kuisema serikali, kuichagiza bali pale serikali, sekta binafsi na wabia wengine wanapofanya vizuri, wanapaswa kupongezwa.

Aidha, alisema masuala ya kuwahusisha wanawake katika maendeleo yalikubalika siku nyingi toka mkutano wa Beijing ambao uliazimia kuwa lazima katika kupanga sera, sheria na mikakati ya nchi kuhakikisha masuala ya jinsia yanakuwa sehemu ya mipango hiyo.

Mkurugenzi huyo alisema zipo changamoto katika vyombo vya habari kuandika habari za jinsia na kuwapa nafasi za uongozi wanawake, kwa kuwa utafiti umebaini ni asilimia 22 pekee ya wanawake ndiyo huwa vyanzo vya habari.

Alisema bado kuna safari ndefu katika kuleta usawa wa kijinsia hasa kwenye vyombo vya habari kwa maana ya kuwa na wanawake wengi viongozi na habari zenye sauti za wanawake.

Awali,  Mratibu wa Gender links Tanzania, Gladness Munuo, alisema alitembelea vyombo vya habari 15 na kuingia makubaliano ya kuangalia umuhimu wa kuwa na sera ya masuala ya jinsia.

Katika mashindano hayo, kazi 115 ziliwasilishwa kati ya hizo 45 ziliingia hatua ya pili ya mashindano, na baadaye walipatikana washindi tisa kutoka kwenye radio, luninga na magazeti.

LOWASA KUZINDUA KAMPENI ZA UCHAGUZI

Waziri Mkuu mstaafu ambaye pia in Mjumbe wa Kamati kuu Chadema, Edward Lowassa atazindua kampeni za uchaguzi mdogo wa Monduli, Jumatano Agosti 29, 2018.

Lowassa atazindua kampeni za Chadema eneo la Mtowambu katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Septemba 16.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Arusha, Aman Golugwa amesema wamejipanga Jumatano Agosti 29 kuzindua kampeni kwa kishindo.

"Tutakuwa na viongozi kadhaa akiwamo Lowassa ambaye ni mbunge mstaafu wa Monduli na tuna uhakika wa ushindi tena Monduli," amesema.

Golugwa amesema chama hicho kinajua michezo michafu ambayo inaendelea kufanywa na CCM, lakini wanataka dunia ijue CCM haikubaliki tena.

"Kuna figisu figisu nyingi hata hizi za wagombea udiwani kupita bila kupingwa lakini wasifikiri Chadema itakufa," amesema.

Katika uchaguzi wa Monduli vyama vinane vinashiriki Chadema wamempitisha kugombea diwani wa Lepurko, Yonas Laizer.

Kata hiyo ndiyo anakotoka Kalanga ambaye pia alikuwa diwani wa kata hiyo hadi mwaka 2015 akiwa CCM na kujiunga na Chadema.

Friday, August 24, 2018

RAIS MAGUFULI AWASHUKURU WATANZANIA BAADA YA MSIBA WA DADA YAKE

 Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewashukuru viongozi na Wananchi wote waliompa pole na waliojitokeza kumfariji wakati wa msiba wa Dada yake mpendwa Bibi. Monica Joseph Magufuli.

Thursday, August 16, 2018

REAL MADRID YAPOKEA KICHAPO CHA MABAO 4-2 DHIDI YA ATLETICO

Real Madrid imekubali kichapo cha mabao 4-2 dhidi ya Atletico de Madrid katika mchezo wa UEFA Super CUP.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa A. Le Coq Arena, Real Madrid walifanikiwa kupata mabao yao yakifungwa na Sergio Ramos kwa njia ya penati na Karim Benzema.

Atletico de Madrid wao wamepata mabao yao kupitia kwa Diego Costa aliyetupia mbili kambani, Saul Niguez na Koke aliyefunga katika dakika ya 104.

OKWI ATOA SALAM HIZI KWA MTIBWA

MABAO mawili yaliyofungwa na Mganda Emmanuel Okwi yaliwafanya mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Arusha United katika mechi ya kirafiki iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid jijini hapa jana,-

ikiwa ni mechi ya mwisho kwa Wekundu wa Msimbazi hao kabla ya kuivaa Mtibwa Sugar Jumamosi.

Okwi alifunga bao la kwanza katika dakika ya saba akimalizia pasi ya Asante Kwasi, huku Ali Kabunda akifanikiwa kuisawazishia timu yake hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza dakika 10 baadaye akitumia makosa yaliyofanywa na mabeki wa Simba katika eneo la 18.

Bao la pili la Okwi lilipatikana katika dakika ya 29 na kuwafanya mabingwa hao wa Bara kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-1 kwenye mchezo huo ambao ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Simba ilikosa bao la wazi katika dakika ya 42 baada ya Hassan Dilunga kupiga shuti pembeni na kupoteza pasi aliyopewa na Okwi, lakini kiungo huyo aliyetokea Mtibwa Sugar alilazimika kutoka nje na nafasi yake kuchukuliwa na Mzambia, Clatous Chama kutokana na kuwa na maumivu yaliyotokana na mchezaji wa Arusha United.

Timu zote zilifanya mabadiliko katika kipindi cha pili, lakini hakuna upande ambao ulifanikiwa kuliona bao la mwenzake huku wachezaji wa Arusha United ambao waliahidiwa zawadi ya Sh. milioni moja kwa kila bao watakalofunga walionekana 'kuamka', hata hivyo jitihada zao hazikuzaa matunda.

Kikosi cha Simba kinatarajia kurejea Dar es Salaam leo kwa ajili ya kujiandaa na safari ya kuelekea Mwanza kuwafuata Mtibwa Sugar katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Pacsal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/ Clatous Chama (dk 44), James Kotei/Mohamed Rashid (dk 56), Meddie Kagere/ Adam Salamba (dk 72), Emmanuel Okwi/ Rashid Juma (dk 81) na Shiza Kichuya/ Mzamiru Yasin (dk 76).

PROFESA KABUDI ATEMA CHECHE DODOMA

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuanzia sasa mawakili walioko kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na wanasheria wote katika Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi za Serikali watakuwa ni Mawakili wa Serikali.

Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatano, Agosti 15, 2018) kabla hajamkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ahutubie wageni waliohudhuria uzinduzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

“Kwa miaka mingi kumekuwa na ombwe la usimamizi wa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma. Maamuzi mengi yamekuwa yakifanyika pasipo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuwa na taarifa. Mambo yanapoharibika ndio Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inataarifiwa ili kuokoa jahazi,” alisema.

Alisema hali hiyo kwa miaka mingi imekuwa ikiisababishia Serikali kuingia kwenye migogoro na kuingia hasara. “Baada ya mabadiliko haya, wanasheria wote walioajiriwa katika utumishi wa umma wanakuwa wanafanya kazi na kutumia mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya wizara zao, taasisi zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa,” alisema.

“Vilevile wanasheria hao watakuwa chini ya uangalizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Nia ya mabadiliko haya ni kumuwezesha Mwanasheria Mkuu wa Serikali awe na usimamizi juu yao na kuwazuia kufanya kazi bila kufuata maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”

Prof. Kabudi alisema mashirika yote ya kimkakati kama vile Bandari, TANESCO nayo pia yataletwa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuepuka kuitia Serikali hasara. “Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mashirika haya, lakini kuna maamuzi yanafanyika wakati Ofisi ya Mwanasheria Mkuu haina taarifa,” amesema.

“Kutokana na  marekebisho hayo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaratibu na kusimamia Mawakili wa Serikali walio katika Ofisi hiyo na wanasheria wote katika Wizara, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi za Serikali ambao sasa watakuwa ni Mawakili wa Serikali. Aidha, Mawakili wa Serikali walio katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali watakuwa chini ya uratibu na usimamizi wa Mkurugenzi wa Mashtaka na Wakili Mkuu wa Serikali,” amesema.

Amesema marekebisho hayo yanatokana na marekebisho ya muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia matangazo ya Serikali Na. 48, 49 na 50 ya tarehe 13 Februari, 2018.

“Leo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kufanya marekebisho hayo. Rais alianzisha Ofisi huru ya Taifa ya Mashtaka kuchukua nafasi ya iliyokuwa Divisheni ya Mashtaka chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Vilevile, Rais alianzisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya madai yakiwemo ya kikatiba ambayo Serikali ni mdaawa ambayo awali yalikuwa yakishughulikiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” amesema.

Amesema marekebisho hayo yanakusudia kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashtaka ya jinai nchini hususani utekelezaji wa azma ya Serikali ya kutenganisha shughuli za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka. “Kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kunalenga kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya madai na pia kuiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuimarika katika weledi na ubobezi wa kitaalamu katika kuishauri Serikali na kuandika Miswada ya Sheria kwa kuzingatia mabadiliko makubwa katika tasnia ya sheria kitaifa, kikanda na kimataifa,” ameongeza.

Hata hivyo, Prof. Kabudi alionya kwamba mabadiliko yoyote hayawezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa kama watendaji hawatabadili mtizamo wao. Ni kweli muundo uliobadilishwa ulikaa kwa miaka mingi na inawezekana mambo mengi yalikuwa yanafanyika kwa mazoea. “Kutokana na mabadiliko haya, tunakiri kuwa mitizamo yetu na ya watumishi wenzetu lazima ibadilike. Tumejipanga kuhakikisha kuwa watumishi hawafanyi kazi kwa mazoea ili wasiwe na tashwishwi wala ajizi katika kutekeleza majukumu ya umma.”

“In public service, learn to swallow your pride. In public service, learn to learn your limits. In public service, learn to obey the authority above you, and if you don’t, resign and quit,” alisisitiza.

“Tumejipanga kufanya kazi kwa weledi na katika hili tutaweka mikakati ya kuwaongezea watumishi wa ofisi hizi ujuzi katika maeneo mahususi, na katika hilo tutaweka mipango ya kuwafanyia placement ndani na nje ya nchi ili wapate ujuzi mahususi na kuhakikisha wanapata mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika maeneo mbalimbali.

Alisema wameanza mkakati wa kuanzisha umoja wa wanasheria walio katika utumishi wa umma ili kuwawezesha kukutana mara kwa mara na kwamba Agosti 30-31 mwaka huu, wanatarajia kufanya mkutano huo ili kuwaunganisha wanasheria wote wajione wanafanya kazi moja na katika Serikali moja.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

MTIBWA SUGAR YAJITAMBA MBELE YA SIMBA

MABINGWA wa Kombe la FA, Mtibwa Sugar wamesema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba watakapokutana katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Ufundi wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga, alisema kikosi chao kipo imara na tayari kwa ajili ya kupambana na Simba ili kuanza vema msimu mpya.

Mayanga alisema wanafahamu ubora na udhaifu ya Simba, hivyo wachezaji wake watakuwa makini kuhakikisha wanashinda na "kuwanyamazisha" mabingwa hao wa Bara wanaonolewa na Mbelgiji Patrick Aussems.

"Tumejipanga vizuri kukutana na Simba katika mchezo huo ambao utakuwa na ushindani mkubwa," alisema Mayanga.

Aliongeza kuwa wanataka kushinda mechi hiyo ili kuwapa furaha mashabiki wao na wanaamini malengo waliyojiwekea ya kutwaa ubingwa wa Bara katika msimu 2018/19 yatatimia.

"Baada ya kumaliza kukutana na Simba hatutapoteza muda na moja kwa moja tutaanza safari ya kuja jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga," alisema Mayanga.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa hawana wasiwasi na mchezaji hata mmoja kutokana na maandalizi ya muda mrefu waliyoyafanya huku pia akitamba safu yake ya ushambuliaji ipo vizuri.

"Tunaupa umuhimu mkubwa mchezo huo, tukiwa na lengo la kulipeleka kombe Manungu," Mayanga aliongeza.