MABINGWA wa Kombe la FA, Mtibwa Sugar wamesema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba watakapokutana katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Ufundi wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga, alisema kikosi chao kipo imara na tayari kwa ajili ya kupambana na Simba ili kuanza vema msimu mpya.
Mayanga alisema wanafahamu ubora na udhaifu ya Simba, hivyo wachezaji wake watakuwa makini kuhakikisha wanashinda na "kuwanyamazisha" mabingwa hao wa Bara wanaonolewa na Mbelgiji Patrick Aussems.
"Tumejipanga vizuri kukutana na Simba katika mchezo huo ambao utakuwa na ushindani mkubwa," alisema Mayanga.
Aliongeza kuwa wanataka kushinda mechi hiyo ili kuwapa furaha mashabiki wao na wanaamini malengo waliyojiwekea ya kutwaa ubingwa wa Bara katika msimu 2018/19 yatatimia.
"Baada ya kumaliza kukutana na Simba hatutapoteza muda na moja kwa moja tutaanza safari ya kuja jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga," alisema Mayanga.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa hawana wasiwasi na mchezaji hata mmoja kutokana na maandalizi ya muda mrefu waliyoyafanya huku pia akitamba safu yake ya ushambuliaji ipo vizuri.
"Tunaupa umuhimu mkubwa mchezo huo, tukiwa na lengo la kulipeleka kombe Manungu," Mayanga aliongeza.
No comments:
Post a Comment