Monday, August 27, 2018

VYOMBO VYA HABARI VINA HAKI YA KUIKOSOA SERIKALI

MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, DK. HASSAN ABBAS.

MSEMAJI Mkuu wa serikali, Dk. Hassan Abbas, amesema vyombo vya habari vina haki ya kuieleza na kuikosoa serikali, sekta binafsi na jamii wanapokosea katika utekelezaji wa majukumu yao mbalimbali.

Aidha, amesema vyombo vya habari visivyofanya hivyo vitakuwa haviitendei haki jamii ambayo inawategemea.

Dk. Abbas ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa sherehe ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari za Jinsia, zilizoandaliwa na Umoja wa Mataifa, linaloshughulikia wanawake (UN Women) kwa kushirikiana na Gender Links.

Tuzo hizo zilitanguliwa na mkutano wa siku mbili wa kujadili masuala mbalimbali ya jinsia, hasa wajibu wa waandishi wa habari na umuhimu wa kuwa na wanahabari wengi ambao ni viongozi kwenye vyombo vya habari, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika nchini.

“Vyombo vya habari vina wajibu mpana katika masuala ya maendeleo, ya jinsia au maendeleo kwa upana wake…vina haki ya kutueleza sisi serikali na sekta binafsi wapi tunakosea kwenye sera, mipango na mikakati yetu ili hatua ziweze kuchukuliwa, wasipotekeleza watakuwa hawajaitendea haki jamii,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Abbas, vyombo vya habari ni muhimili wanne ambao unapaswa kutekeleza wajibu huo kwa kuangalia kama serikali na jamii kwa ujumla wanazingatia masuala ya jinsia na usawa wa wanawake.

“Vyombo vya habari ni wabia, wasibakie kuwa viranja na kutazama tu, pale wanapopaswa kuingia uwanjani na kucheza, basi huo ni wajibu wao pia wanakaribishwa,” alisisitiza.

Alisema vyombo hivyo visibaki kwenye kuisema serikali, kuichagiza bali pale serikali, sekta binafsi na wabia wengine wanapofanya vizuri, wanapaswa kupongezwa.

Aidha, alisema masuala ya kuwahusisha wanawake katika maendeleo yalikubalika siku nyingi toka mkutano wa Beijing ambao uliazimia kuwa lazima katika kupanga sera, sheria na mikakati ya nchi kuhakikisha masuala ya jinsia yanakuwa sehemu ya mipango hiyo.

Mkurugenzi huyo alisema zipo changamoto katika vyombo vya habari kuandika habari za jinsia na kuwapa nafasi za uongozi wanawake, kwa kuwa utafiti umebaini ni asilimia 22 pekee ya wanawake ndiyo huwa vyanzo vya habari.

Alisema bado kuna safari ndefu katika kuleta usawa wa kijinsia hasa kwenye vyombo vya habari kwa maana ya kuwa na wanawake wengi viongozi na habari zenye sauti za wanawake.

Awali,  Mratibu wa Gender links Tanzania, Gladness Munuo, alisema alitembelea vyombo vya habari 15 na kuingia makubaliano ya kuangalia umuhimu wa kuwa na sera ya masuala ya jinsia.

Katika mashindano hayo, kazi 115 ziliwasilishwa kati ya hizo 45 ziliingia hatua ya pili ya mashindano, na baadaye walipatikana washindi tisa kutoka kwenye radio, luninga na magazeti.

No comments:

Post a Comment