Nchini pia mambo ni hivyo hivyo, usajili umekuwa ukipamba moto.
Kila klabu inasaka wachezaji ambao inaona kuwa itawasaidia kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/19.
Tayari Shirikisho la Soka nchini (TFF), limeshafungua dirisha la usajili tangu Juni 15 na linatarajiwa kufungwa Julai 26, mwaka huu.
Wafuatao ni wachezaji kutoka ndani na nje ya nchi ambao tayari wameshatua kwenye klabu mpya na kuthibitishwa rasmi.
1. Donald Ngoma-Azam FC
Straika huyu hatari wa zamani wa Yanga raia wa Zimbabwe, ametua kwenye klabu ya Azam FC. Ingawa imeelezwa bado ana majeraha, lakini wakati ligi itakapokuwa imeanza atakuwa amebakisha wiki chache kati ya zile alizotakiwa kupumzika kwa mujibu wa madaktari wake.
2. Tafadza Kutinyu-Azam FC
Ni Mzimbabwe mwingine aliyetua kwenye klabu ya Azam FC kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu. Huyu naye si mgeni sana masikioni mwa mashabiki wa soka, kwani msimu uliomalizika alikuwa akiichezea Singida United.
3. Meddie Kagere-Simba
Ni mzaliwa na Uganda mwenye uraia wa Rwanda. Ni mmoja wa mastraika hatari kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Straika huyo amesajiliwa na klabu ya Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya. Ameanza kuonyesha cheche zake kwenye michuano ya Kagame inayoendelea.
4. Tiba John-Singida United
Anacheza kama kiungo wakati mwingina straika. Msimu uliomalizika alikuwa akiichezea Ndanda FC. Lakini msimu ujao wa ligi mashabiki watamuona akiwa ametinga uzi wa timu ya Singida United. Tayari ameanza kung'ara kwenye Kombe la Kagame.
5. Adam Salamba-Simba
Msimu uliomalizika alichezea timu mbili. Nusu msimu wa kwanza alikuwa na Stand United, kabla ya kujiunga na Lipuli kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu iliyomalizika.
Kwa sasa amesajiliwa na Simba kwa ajili ya msimu ujao. Ameshaanza kuichezea timu hiyo kwenye michuano mbaliambali; ya SportPesa Super Cup nchini Kenya na Kagame Cup inayoendelea nchini.
6. Juma Kaseja-KMC
Ni kipa wa zamani wa klabu za Simba na Yanga na hata Mbeya City. Msimu uliomalizika alikuwa akiidakia Kagera Sugar na kufanya vizuri.
Mkongwe huyo kuelekea msimu ujao amesajiliwa na timu iliyopanda daraja msimu huu ya KMC ya Kinondoni.
7. Eliuter Mpepo-Singida United
Huyu alikuwa ni straika tegemeo kwenye timu ya Prisons ya Mbeya.
Kwa sasa amejiunga na Singida United na tayari ameanza kuichezea timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Kagame.
8. Yusuph Ndikumana-KMC
Klabu ya KMC iliendelea kushangaza wengi, kwani baada ya kumsajili Kaseja, ikamsajili beki kisiki wa Mbao FC, Yusuph Ndikumana. Msimu uliopita timu za Simba na Yanga zilishindwa kumsajili kutokana na dau lake kuwa kubwa.
9. Habib Kyombo-Singida United
Alitwaa tuzo ya straika kijana kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara. Msimu huu amejiunga na Singida United, akitokea Mbao FC. Ni mmoja wa mastraika hatari na tegemeo baadaye nchini.
10. Sadala Mohamed-KMC
Ni beki aliyekuwa akiitumikia Mbao FC, lakini kwa sasa tayari ameshatua kwenye klabu ya KMC kwa ajili ya kuichezea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao wa ligi.
11. Mohamed Rashid-Simba
Alikuwa straika wa kutumainiwa na Prisons ya Mbeya msimu uliomalizika. Msimu huu amejiunga na mabingwa wapya Simba na tayari wanachama na mashabiki wa timu hiyo wameshamshuhudia kwenye mechi mbalimbali, zikiwamo za Kombe la Kagame.
12. Marcel Kaheza-Simba
Alikuwa na msimu mzuri uliomalizika, akiichezea timu ya Majimaji ya Songea. Msimu ujao ataonekana akiwa amevaa uzi wa Simba.
Tayari wanachama na mashabiki wa timu hiyo wameshaanza kumshuhudia kwenye michuano ya Kombe la Kagame.
No comments:
Post a Comment