Tuesday, June 12, 2018

ZAHERA KUJADILIWA NA KAMATI


SIKU moja baada ya kuundwa kwa Kamati ya Mpito ndani ya Klabu ya Yanga, moja ya mambo ambayo itayafanyia kazi ni kujadili uwezo wa kocha wao mpya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),

Mwinyi Zahera kama anastahili au hastahili kuwapo kwenye kikosi hicho kinachoshiriki mechi za hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

 Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Ridhiwani Kikwete alisema kuwa wakati wanaanza na mchakato wa kupitia mikataba ya wachezaji, pia wataufanyia kazi wasifu wa Zahera ambaye alitua nchini kuchukua mikoba iliyoachwa na Mzambia, George Lwandamina.

Ridhiwani alisema kuwa pia kamati yao itasaka kocha msaidizi ambaye ataungana na kocha mkuu kukinoa kikosi cha wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobakia kwenye mashindano ya kimataifa na kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Hapa ndio kwenye msingi wa mafanikio na tunahitaji  umakini zaidi, tunahitaji kujua wachezaji watakaobaki na watakaoondoka, tunataka kuirejesha timu yetu kwenye ushindani na hadhi yake," alisema Ridhiwani ambaye kwa taaluma ni mwanasheria.

Alisema pia kamati hiyo itapitia upya maslahi ya walimu wengine walioko kwenye benchi la ufundi kwa sababu wanahitaji kuona kila idara inaimarika na kutekeleza majukumu kwa kiwango cha juu.

"Kwanza jambo la furaha ni kuwa wajumbe wote tulioteuliwa katika kamati hiyo tumepigiwa simu na kukubali jukumu tulilokabidhiwa, tunasubiri wito wa kikao baada ya mwenyekiti (Abbas Tarimba) na makamu wake  kukutana kupanga kikao ili tuanze kazi hii haraka," alisema mjumbe huyo ambaye aliwahi kuvuliwa uanachama wa klabu hiyo baada ya kutofautiana na uongozi.

Aliongeza pia wao kama wanachama wa Yanga watapata nafasi ya kutoa ushauri baada ya klabu yao kukubali kubadili mfumo wa uendeshaji kwa kuwasilisha maoni yanayofaa kwa kamati iliyochaguliwa ambayo iko chini ya mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa.

Yanga kwa sasa iko mapumziko na itaanza mazoezi Juni 25 mwaka huu kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia ya Kenya ambao utafanyika ugenini Julai 18 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment