Tuesday, June 12, 2018

DONALD NGOMA AGUNDULIKA AMECHANIKA MTULINGA WA GOTI LA MGUU

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imethibitisha rasmi kuingia kandarasi ya mwaka mmoja na mshambuliaji Donald Ngoma hapo jana siku ya Jumatatu atakaoanza kuutumikia kuanzia msimu ujao baada ya vipimo vyake kukamilika na kugundulika kuwa amechanika mtulinga.

Zoezi hilo la vipimo lilienda vema kwenye Hospitali ya Vincent Pallotti nchini humo, ambapo imegundulika amechanika mtulinga wa mbele wa goti la mguu wa kulia (Anterior Crusiate Ligament), majeraha yatakayomweka nje hadi Agosti 11 mwaka huu atakaporuhusiwa kucheza mechi za ushindani.

Awali pande hizo mbili ziliingia makubaliano ya mkataba huo (memorandum of understanding) kwa sharti la kumfanyia vipimo vya afya jijini Cape Town, Afrika Kusini kujua undani wa majeraha ya goti aliyokuwa nayo.

Meneja wa timu hiyo, Phillip Alando ameiyambia tovuti ya klabu hiyo kuwa tayari wameingia mkataba na mshambuliaji huyo hatari kutoka nchini Zimbabwe baada ya kuridhishwa na ripoti za vipimo kutoka kwa wataalamu nchini Afrika Kusini.

“Nathibitisha kuwa leo (jana) tumeingia mkataba rasmi na Ngoma (Donald), mashabiki watambue ya kuwa mchezaji huyo atakuwa ni miongoni mwa wachezaji wapya watakaovaa jezi ya Azam FC msimu ujao, hakuna asiyemfahamu Ngoma, anaijua vema ligi yetu na changamoto ya mechi za kimataifa hivyo tunatarajia mambo mazuri kutoka kwake,” amesema Alando.

Tayari Ngoma ameshakabidhiwa jezi namba 11 aliyokuwa akitumia kwenye timu yake ya awali ya Yanga, ambapo usajili wake ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu mpya, Hans Van Der Pluijm aliyewahi kufanya naye kazi pamoja akiwa kwa Wanajangwani hao.

Ngoma, 28, anaungana na Mzimbabwe mwenzake Tafadzwa Kutinyu, ambaye naye ameshasaini kuitumikia Azam FC msimu ujao akitokea Singida United, raia mwingine wa taifa hilo aliyeko kwenye kikosi hicho ni beki wa kushoto, Bruce Kangwa, atakayekuwa akiitumikia timu hiyo kwa msimu wa tatu.

No comments:

Post a Comment