Wednesday, May 2, 2018

TASAF YARINGIA MAFANIKIO KATIKA MIRADI YA KUPAMBANA NA UMASIKINI NCHINI

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF umefanikiwa kutekeleza miradi 14,051 yenye thamani ya shilingi bilioni 502 Tanzania Bara na Zanzibar tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999/2000. 

Akitoa taarifa kwa ujumbe wa Maafisa wa Shirika la Misaada la Maendeleo la Sweden-SIDA waliotemebelea ofisi za TASAF jijini Dar es salaam na kisha kutembelea eneo la Makangarawe,katika Wilaya ya Temeke,Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bwana Ladislaus Mwamanga ametaja miradi iliyotekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Elimu, Afya,Maji, Barabara, Hifadhi ya Mazingira, Kilimo ,ufugaji n.k ambayo ilitekelezwa kwa mafanikio makubwa kwa kuwashirikisha wananchi kwenye maeneo yao. 

Bwana Mwamanga amesema kutokana na Mafanikio ya awamu ya I na II ya TASAF, Serikali iliamua kuanzisha awamu ya III ambayo kwa kiwango kikubwa inajielekeza katika kuzikwamua Kaya zinazokabiliwa na umaskini uliokithiri baada ya kugundua kuwa hazikuwa zinanufaika na huduma zilizokuwa zinapatikana kwenye maeneo yao kutokana na umaskini. 

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF ameuambia ujumbe huo kutoka SIDA kuwa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umeanza kuonyesha mafanikio na Walengwa wameanza kuwekeza katika miradi ya kiuchumi na hivyo kujiongeza kipato chao hususani katika nyanja za kilimo,mifugo na ujenzi wa nyumba huku suala la elimu na afyakwa watoto wao likipewa kipaumbele. 

Amesema hadi sasa TASAF inahudumia takribani kaya MILIONI MOJA NA LAKI MOJA ambazo zimeendelea kupata ruzuku na huduma nyingine kama elimu ya ujasiliamali, hifadhi ya mazingira,lishe, huku mkazo pia ukielekezwa katika kuhamasisha walengwa kuunda vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana ili kukuza shughuli za kiuchumi kwenye maeneo yao. 

Ujumbe huo kutoka SIDA baada ya kupata taarifa pia ulipata fursa ya kuuliza maswali juu ya Utekelezaji wa shughuli za Mpango na kujibiwa na Viongozi wa TASAF na kisha kuelekea katika eneo la Makangarawe,katika wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam ambako ulikutana na baadhi ya vikundi vya Walengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini na kujionea biadhaa mbalimbali zinazotengezwa na walengwa hao kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato. 

Hata hivyo katika maelezo yao,Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini huko Makangarawe wameonyesha kukabiliwa na tatizo la upatikanaji wa soko la bidhaa wanazozitengeneza huku pia wakiomba kupatiwa eneo mahususi kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao kwa ufanikisi.

No comments:

Post a Comment