Tuesday, March 13, 2018

YANGA YAELEKEA BOTSWANA KWAAJILI YA MCHEZO WA MAREJEANO

Klabu ya soka ya Yanga imeondoka nchini usiku wa kuamkia leo kuelekea jijini Gaborone nchini Botswana, kwaajili ya mchezo wa marejeano, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers.

Yanga inakwenda Botswana ikiwa na rekodi ya kushinda mechi 8 mfululizo za ligi kuu, huku katika michezo yake 11 iliyocheza ndani ya mwaka 2018 kwenye mashindano yote imeshinda mechi 9 na kutoa sare mechi 1 huku ikipoteza moja dhidi ya Township Rollers.

Katika mchezo huo utakaopigwa Jumamosi ya Machi 17 Yanga inahitaji kupata ushindi wa mabao 2-0 au zaidi ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Msafara wa mabingwa hao wa Tanzania unaongozwa na viongozi 11 huku wachezaji watakaokuwa na jukumu la kuibebea Yanga wakiwa ni 20. Morali ya wachezaji wa Yanga huenda imeongezwa na matokeo ya jana kwenye ligi, ilipoifunga Stand United mabao 3-1 na kufikisha alama 46 sawa na vinara Simba.

Endapo Yanga itafanikiwa kuiondoa Township Rollers itaingia kwenye hatua ya makundi ambapo itajihakikishia kitita cha shilingi bilioni 1.1 kutoka CAF. Kwenye mchezo wa kwanza jijini Dar es salaam Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment