Tuesday, March 13, 2018

BARAZA LA WAZEE CHADEMA LAMSHUKIA RAIS MAGUFULI

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kwa Baraza lake la Wazee wametoa tamko lao la kumtaka Rais John Magufuli kuchukua hatua dhidi ya hali inayoendelea hivi sasa nchini ya kisiasa, kiuchumi kabla ya Taifa kuingia katika mtafaruku.

Akizungumza Makao Makuu ya Chama hicho, Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Rodrick Lutembeke alisema hii ni mara ya pili wanamkumbusha Rais tangu wafanye hivyo mwishoni mwa mwaka jana ambapo walitoa mifano ya mauaji, kuteswa na kushambuliwa kwa wananchi wa kada tofauti.

" Katika tamko letu la awali tulizungumzia mambo kadhaa ikiwemo uminywaji wa demokrasia kwa maana ya vyama vya siasa kuzuiliwa kufanya shughuli zake za kisiasa, bunge kutooneshwa, mahakama kuingiliwa na serikali pamoja na mauaji dhidi ya raia pamoja na kufungiwa kwa vyombo vya habari," alisema Lutembeke.

Amesema yapata miezi sita tangu watoe tamko hilo lakini bado yale ambayo waliyaoanisha katika tamko lao yameendelea kutokea huku hali ikizidi kuwa mbaya ambapo aliyarejea matukio yaliyotokea ndani ya kipindi hicho ikiwemo tukio la kupotea kwa Mwandishi wa Mwananchi, Azory Agwanda, kuuwawa kwa Katibu wa Chadema Kata ya Hananasif, Daniel John pamoja na suala ka kuhusishwa kutekwa kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini, Abdul Nondo.

" Jambo ambalo linatuumiza sana sisi wazee, kama wote mlifuatilia kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu) mbele ya Rais ambapo alizungumza kwa kebehi sana kuwa kijana (Nondo) huyo alijiteka wakati wote tunafahamu vyombo vya Serikali hasa Polisi wakitueleza kuwa bado wanafanya uchunguzi, sasa sijui tutazamie nini juu ya upelelezi huo kwa Polisi wakati waziri mwenye dhamana ameshatoa hukumu.

" Sisi kama wazee hatutonyamaza kimya tutaendelea kupaza sauti yamkini watasikia, tunatoa ushauri kwa Rais achukue hatua dhidi ya haya yanayoendelea nchini, wasipuuzie vilio vya wananchi na wakiendelea na kauli zao hizi wataishia kupelekwa katika mahakama ya kimataifa ya ICC," Amesema Lutembeke.

Amesema waoa wanashauri Rais Magufuli aongozwe na busara na hekima na kukubali kuitikia wito wa kukutana na wazee katika kikao cha pamoja ili wamuambie ukweli ili Taifa liepukane na janga lililopo.

Amemtaka Rais Magufuli kukubali kukosolewa kama ambavyo amekuwa akikubali kusifiwa. " Kama ambavyo amejiona ana sifa kubwa ambazo anaweza hata kuongoza malaika basi akubali kukosolewa na kushauriwa pia," amesema Lutembeke.

No comments:

Post a Comment