Sunday, February 11, 2018

WAZIRI MWAKYEMBE AZIVULIA KOFIA SIMBA NA YANGA


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameridhishwa na kiwango cha Simba jana katika michuano ya kimataifa na kukiri kuwa kwasasa Tanzania sio kichwa cha Mwendawazimu tena.

Akiongea mbele ya wanahabari Mwakyembe alieleza furaha yake kuona timu mbili zinazoiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya kimataifa Yanga SC na Simba SC zikiibuka na ushindi katika mechi zake za kwanza.

''Kama kiwango cha mpira wa miguu Tanzania kitakuwa hiki, basi sisi sio tena kichwa cha Mwendawazimu kwasababu kiwango cha timu hizi kinaonesha kweli timu zimekuwa kambini na zina walimu wazuri, sisi ni kichwa cha Muungwana'', amesema.

Yanga inaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika ambapo katika mchezo wake wa hatua ya awali jumamosi iliyopita iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya St. Louis ya Shelisheli.

Simba wenyewe wanaiwakilisha nchi katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika ambapo jana imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Gendarmerie ya Djibouti.

No comments:

Post a Comment