Edward Lowassa.
Wazri mkuu mstaafu, Edward Lowassa amesema kuwa anawakaribisha Chadema wale wote waliokatwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Alhamisi, Lowassa amesema, “Nimesoma na kusikia baadhi ya waliokuwa viongozi katika Chama Cha Mapinduzi wamekatwa ama kutetea nafasi zao au kugombea, kwa sababu mbalimbali. Na jina langu limekuwa likiendelea kutajwa tajwa humo,”
“Mimi nawaambia hawa Watanzania wenzetu waliokatwa huko CCM nawakaribisha huku Ukawa wafurahie demokrasia. Huku niliko kuna maisha mazuri ya kisiasa, uhuru wa fikra na demokrasia halisi.”
Lowassa amesema Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alisema ni wakati muafaka kwa Tanzania kuwa na mfumo wa vyama vingi, pamoja na kwamba maoni ya Watanzania wengi wakati ule kupitia tume ya Nyalali (Jaji Francis) kutaka kuendelea na mfumo wa chama kimoja.
“Nataka kuwakumbusha Watanzania wenzangu hawa, uamuzi ule wa Baba wa Taifa, ulilenga kuwapa Watanzania demokrasia ya kuwa na uwanja mpana wa kufanya siasa,”
“Mimi nimetumia fikra hizo za mwalimu na hakika hivi sasa ninafurahia demokrasia halisi huku niliko. Kwa wote waliokatwa na wanahisi wameonewa waondokane na unyonge wa fikra kudhani kuwa bila CCM hakuna maisha… waje huku tufanye siasa kwa manufaa ya wananchi wetu.”
Lowassa amewaomba Wana-Chadema wenzake kuwapokea kwa mikono miwili na wale wanaoendelea kubaki huko CCM waendelee kushikamana hadi uchaguzi mkuu ujao 2020 ambapo upinzani utakapoonyesha makucha yao.
“Vitisho na nguvu ya dola inayotumika kujaribu kutunyamazisha sisi wa upinzani isiwatishe wala kuwaongofya hata mara moja.”
No comments:
Post a Comment