Tangu miaka ya 1990 kumekuwa na mipango mbalimbali ya kuboresha usafiri Dar es Salaam ikiwamo kuanzisha barabara za aina mbalimbali, kama za mabasi yaendayo kasi, maegesho ya magari ya kulipia na kuhamasisha kujengwa kwa majengo yenye maegesho ya magari.
Pamoja na jitihada za serikali ya jiji na serikali kuu kuboresha usafiri bado kuna kero kubwa ya usafiri wa abiria, hasa wakati asubuhi na jioni hali inayowalazimu wananchi kuchukua takribani saa tatu barabarani badala ya dakika 15 hadi 30 , kwa mfano, kutoka Mbezi ya Barabara Morogoro hadi katikati ya jiji na Kariakoo.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, tangu mwaka 2008 Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam imetekeleza miradi maalum ya ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano katika barabara kuu za jiji.
Mhindisi Miradi wa Ofisi ya Tanroads Mkoa wa Dar Es Salaam, Julius Ngusa, anasema mradi wa ujenzi wa barabara za pembezoni wa awamu ya tatu ni moja ya mikakati ya serikali ya kushughulikia tatizo sugu la msongamano wa magari ambapo utekelezaji wake ulianza tangu 2008/2009.
Anasema kupitia mradi huo, serikali ilichagua barabara tisa kwa ajili ya kujengwa katika viwango vya lami nazo ni barabara ya Ubungo (bus terminal)-Kigogo-Kawawa yenye kilometa 6.4, barabara ya Jet Corner-Vituka-Davis Corner urefu wa kilometa 12, nyingine ni Kinyerezi-Kifuru-Msigani-Mbezi Mwisho yenye kilometa 10.
Barabara ya Mbezi- Goba- Tangibovu yenye kilometa tisa, kadhalika ya Kimara Baruti-Msewe-Changanyikeni yenye urefu wa kilometa 2.6.
Ngusa, anazitaja barabara nyingine kuwa ni pamoja na Tegeta Kibaoni-Wazo Hill-Goba-Mbezi ndani ya Morogoro yenye kilometa 20, Kigogo Roundabout-Jangwani-Twiga katika bonde la Msimbazi ikiwa na kilometa 2.72.
Anazungumzia pia Tabata Dampo-Kigogo na Ubungo Maziwa- Mabibo External inayoingia Mandela inayojengwa kilometa 2.25 za lami.
“Miradi hiyo inajengwa katika awamu tatu za utekelezaji, ambapo hadi sasa awamu ya kwanza ya miradi hiyo iliyohusisha ujenzi wa barabara zenye jumla ya kilometa 19.42 tayari imekwishatekelezwa na kukamilika tangu 2008.”
Anaitaja miradi iliyokamilika kuwa ni pamoja na barabara ya Ubungo-Kigogo-Kawawa iliyokamilika mwaka 2010 kwa gharama ya Sh bilioni 11.44, Kigogo-Msimbazi-Jangwani iligharimu bilioni 7.64 ambayo ilikamilika mwaka 2017 pamoja na barabara ya Jet Corner-Vituka-Devis Corner iliyomalizika mwaka 2011.
“Kuhusu awamu ya pili yenye urefu wa kilometa 27.5 na ujenzi wa daraja la Kinyerezi lenye urefu wa mita 40, kazi ilianza mwaka 2014 ambako hadi sasa zilizojengwa kwa kiwango cha lami ni pamoja na barabara ya Tangi Bovu (Samaki)-Goba iliyomalizika mwaka jana na kugharimu bilioni 8.6 ” anasema Ngusa.
Katika awamu hiyo mwaka 2016 serikali pia ilikamilisha ujenzi wa Barabara ya Tegeta Kibaoni-Wazo Hill-Goba-Mbezi Mwisho yenye kilometa 20, kwa gharama ya Sh bilioni 6.7.
Akifafanua zaidi Ngusa anasema miradi mingine iliyokamilika ni pamoja na Barabara ya Kilungule (Maji Chumvi)- External/Mandela yenye kilometa 3.3, ambapo mradi huo ulikamilika mwaka 2015 kwa gharama ya Sh. bilioni 4.4.
Aidha mradi wa barabara ya Kimara Baruti-Msewe wenye kilometa 2.6 uliopaswa kukamilika mwaka jana umeshindishwa kuisha kwa wakati kutokana na kutokuwepo kwa nafasi ya kujenga barabara, ambapo hata hivyo hadi kufikia 30 Septemba, 2017 mradi huo ulijengwa kwa asilimia 80.
Mhandisi Ngusa anasema awamu ya tatu ya utekelezaji wa miradi hiyo ulioanza mwaka 2016 na 2017 unahusika ujenzi wa barabara za Kifuru-Msigani, Goba-Makongo na Goba-Madale zenye urefu wa kilometa 14.1 na unatarajia kukamilika mwanzoni na nyingine mwishoni mwa mwaka 2018.
“Miradi ya barabara ya Goba-Madale na Goba-Makongo hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu imekamilika kwa asilimia 52 wakati ule wa Kifuru-Msigani umefikia asilimia 87, malengo ni kuhakikisha kuwa miradi hii inamalizika kwa wakati kwa kuzingatia ubora na viwango tulivyojiwekea” anasema Ngusa.
Baadhi ya changamoto inayokabili miradi hiyo ni pamoja na wamiliki wa nyumba nyingi kuhitaji fidia, ambapo Tanroads kwa kushikiana na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) zimeanza uthamini na malipo yatalipwa na Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Anasema serikali pia inaendelea na ujenzi wa barabara za Msongola-Mbande zenye kilometa moja nyingine ni Ununio-Mbweni urefu wa kilometa moja pia , Kitunde-Kivule yenye urefu wa kilometa 3.2, pia kilometa nyingine moja zinajengwa za barabara ya Dege-Gomvu.
Kukamilika kwa miradi hii kutaongeza tija na ufanisi katika kuchochea kasi ya maendeleo ya Dar es Salaam na taifa .