Tuesday, October 3, 2017

MAREKANI YAINYA MVUTANO UNAOENDELEA KENYA

Nchi za Marekani na Uingereza zimeingilia kati mvutano wa kisiasa unaoendelea baina ya Chama cha Jubilee na Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA) kuhusu uchaguzi wa Rais nchini Kenya kwa kuzitaka pande zinazohusika ziondoe masharti waliyoweka na zizungumzie kupata mwafaka.Balozi wa Marekani nchini Kenya, Robert Godec na Naibu Balozi wa Uingereza nchini humo, Susie Kitchens wamekaririwa wakisema kuwa, uchaguzi wa marudio usipofanyika Oktoba 26 mwaka huu, kutakuwa na mgogoro wa kikatiba kwenye nchi hiyo. Mwishoni mwa wiki, Katibu wa mgombea urais kupitia Nasa, Dennis Onyango alisema mwanasiasa huyo Raila Odinga na mabalozi walizungumzia masuala kadhaa, lakini kubwa zaidi ni mvutano kuhusu uchaguzi wa marudio wa Rais, muswada wa mabadiliko ya sheria za uchaguzi na kinachoendelea katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC).

Wanadiplomasia hao wamekaririwa kusema kuwa, masharti mengi yaliyotolewa hayatekelezeki kwa kuwa muda hautoshi. NASA wametoa masharti kadhaa likiwemo la kufukuzwa kwa maofisa 10 wa IEBC akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Ezra Chiloba. NASA pia wanataka zabuni zilizotolewa kwa kampuni ya Al-Ghurair inayochapisha karatasi za kupigia kura, na kampuni ya masuala ya teknolojia ya Safran Morpho zisitishwe.
Muungano huo pia unashinikiza muswada wa mapendekezo ya marekebisho ya sheria za uchaguzi yaliyowasilishwa bungeni kwa pendekezo la Jubilee yaondolewe. NASA wamesema, kama masharti yao hayatatekelezwa hawatashiriki kwenye uchaguzi Oktoba 26 na wataandamana kila Jumatatu na Ijumaa kushinikiza yatekelezwe.
Kiongozi wa chama chenye wabunge wengi katika Bunge la Seneti, Kipchumba Murkomen, amesema, wanadiplomasia hao wanataka uchaguzi ufanyike kwa amani na mwanasiasa yeyote asifanye vurugu Mgombea Mwenza wa Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi wa Rais, William Ruto amesema mgombea urais kupitia muungano huo, Raila Odinga hana mamlaka ya kuzuia Wakenya wasipige kura Oktoba 26, mwaka huu.
Amemtaka Raila aache kuwapotosha Wakenya kwamba uchaguzi hautafanyika siku hiyo. Wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi, Raila alisema mapendekezo ya marekebisho ya sheria za uchaguzi ni kuishambulia demokrasia na Katiba hivyo lazima yapingwe.

No comments:

Post a Comment