Tuesday, September 5, 2017

LIL WAYNE ALAZWA HOSPITALI KWA KUUGUA KIFAFA

Mwanamuziki wa nyimbo za kufoka Lil Wayne

Mwanamuziki Lil Wayne amekimbizwa hospitalini baada ya kuanguka kutokana na kifafa na kupatikana akiwa hana fahamu katika chumba cha hoteli alimokuwa huko Chicago.

Mtandao wa wasanii wa TMZ umesema mwanamuziki huyo wa nyimbo za kufoka, 34, anayeugua ugonjwa wa kifafa, ameangushwa na ugonjwa huo mara kadhaa na alipoteza fahamu pindi tu alipowasili huko A&E.

Alitarajiwa kuwatumbuiza mashabiki wake huko Las Vegas siku ya Jumapili usiku.

Nyota huyo, ambaye kwa jina lake rasmi Dwayne Michael Carter Jr, alipokea matibabu mwaka uliopita baada ya kupoteza fahamu mara mbili lakini kwa kiasi kidogo.

Miaka minne iliyopita Lil Wayne alikuwa akipokea matibabu kwa siku kadhaa katika hospitali moja huko Los Angeles.

Baada ya kupata fahamu, mwanamuziki huyo aliambia kituo cha redio cha Power 106 kwamba, anaugua ugonjwa wa kifafa na yuko katika hatari za kukosa fahamu mara kadhaa.

Alimwambia DJ Felli Fel: ''Hiyo haikuwa mara yake ya kwanza, pili, tatu, nne , tano, sita au saba … nimepatwa na kifafa mara kadhaa, ni vile huwa hampati habari hizo.''

Lil Wayne amesema hupoteza fahamu baada ya kupatwa na msongo wa kiakili, kutopumzika na kufanya kazi kupita kiasi.

Mashabiki waliokuwa na wasiwasi wamekuwa wakituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter kupitia #prayforweezy baada ya kisa cha mwanamuziki huyo kuripotiwa.

Mzaliwa huyo wa New Orleans, alianza taaluma hiyo akiwa na umri wa miaka 9, alipokuwa msanii mdogo kusajiliwa na rekodi ya Cash Money.

Tuzo zake tano bora za Grammy zinajumuisha tuzo ya albamu bora ya nyimbo za rap mwaka 2008 kwa albamu yake ya Tha Carter III na utumbuizaji bora wa rap kwa wimbo wake wa No Problem akiwa na Chance the Rapper & 2 Chainz.

No comments:

Post a Comment