Monday, September 4, 2017

ASKARI YA FFU AKAMATWA SAKATA LA UTEKAJI WATOTO

Wakati Mtuhumiwa wa matukio ya utekaji watoto, Samsom Petro (18), ambaye jana alifikishwa Arusha kwa ajili ya kuonyesha sehemu alipowaficha watoto, amebainika kuwa anaishi na kaka yake ambaye ni askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha mjini hapa.

Inadaiwa kuwa askari huyo pia anashikiliwa na polisi kwa mahojiano tangu Agosti 27 wakati kikosi maalum cha polisi kilipozingira nyumba aliyopanga.

Petro, ambaye alikamatwa juzi akiwa Katoro mkoani Geita, anatuhumiwa kuwateka watoto wawili, Moureen David(6) na Ikram Salim(3) na hadi jana jioni alikuwa ameandamana na polisi katika eneo la Njiro ambako alidai aliwatelekeza watoto hao.

Lina Kajuna ambaye ni mmiliki wa nyumba ya aliyekuwa amepanga askari huyo wa FFU, alisema ana miaka miwili tangu ampangishe.

Kajuna alisema mtuhumiwa wa utekaji, Samson Petro alifika Arusha mwezi Juni na amekuwa akiishi na kaka huyo na tangu amefika amekuwa akimuona kuwa na tabia ambazo sio nzuri, kama wizi wa kuku.

“Alipofika muda mfupi tulianza kuona matukio ya wizi nikaibiwa kuku na pesa mimi nikamlalamikia kaka yake lakini akasema tuendelee kumchunga,”alisema

Alisema baada ya hali ya wizi kuendelea, alikwenda kulalamika kwa balozi wa eneo wanaloishi ambalo ni Mtaa wa Olkeria, Daniel Kichau kutaka wamchunguze.
 
Hata hivyo, alisema wakati akichunguza, ndio matukio ya utekaji yakaanza na tangu Agosti 25 alitoweka nyumbani hadi jana walipopata taarifa kuwa amekamatwa.
 
Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa Mtaa wa Olkerian, Daudi Safari alisema jana kuwa kikosi chao cha wananchi walifika kwenye nyumba hiyo na kubaini alikuwa anaishi na askari huyo wa FFU .
 
“Tumemuhoji mama mwenye nyumba ametupa ushirikiano mkubwa na ni kweli Samson alikuwa anaishi kwenye nyumba yake na kaka yake ambaye alikamatwa tangu Agosti 27,” alisema.
 
Katika msako wa jana, polisi walikwenda peke yao na mtuhumiwa na kuwaacha wazazi wa watoto hao wakiwasubiri kituo kikuu cha polisi. Baadhi ya askari walisema wanaendelea na msako wa watoto hao

No comments:

Post a Comment