Friday, August 4, 2017

WATANO WAUAWA KWA UJAMBAZI

Watu watano wameuawa katika matukio mawili ya ujambazi kwenye mikoa ya Kigoma na Katavi.

Taarifa za Kipolisi zinasema kwamba majambazi wanne waliuawa na watu watatu wakijeruhi wakati wa majibizano kati ya Polisi mkoani Katavi na majambazi katika Kijiji cha cha Kahenze, Kata ya Ugala wilayani Mpanda.

Majibizano hayo yalichukua robo saa. Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Benedict Mapujila alisema marehemu hao walikutwa na silaha mbili za vita aina ya SMG zenye namba za usajili UA 5538, 1997 na AFV 0826, 1996 zikiwa na jumla ya risasi 27 katika magazine zake.

Kaimu Kamanda Mapujila amesema kwamba majina ya marehemu yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi. Imeelezwa na Mapujila kuwa siku moja kabla ya kuuawa kwao watu hao wanne walimpora mfanyabiashara, Shija Masanja pesa taslimu shilingi laki nane na simu mbili aina ya Tecno.

Nako Mkoani Kigoma, mtu mmoja amekufa na wengine watatu wamejeruhiwa katika tukio la ujambazi kutokana na gari walilokuwa wakisafiria kushambuliwa kwa risasi ikiwa ni jaribio la kuliteka gari hilo. Tukio hilo lilitokea jana katika Kijiji cha Narulanga Wilaya ya Kibondo, ambako gari dogo la abiria (maarufu kama mchomoko) lenye namba za usajiri T415 DHM lililokuwa linaendeshwa na dereva Miraj Seif (28) lilishambuliwa wakati likitoka Kasulu kwenda Kibondo.

Mkuu wa Wilaya Kibondo, Luis Bura alithibitisha kutokea kwa shambulio hilo na kwamba vikosi vya ulinzi na usalama vimeanza msako wa kuwatafuta majambazi hao huku hatua za kudhibiti vitendo vya ujambazi zikiendelea kuimarishwa.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya hiyo, Kizito Luamvya alisema alipokea watu wanne waliokuwa na majeraha kwenye miili yao na kwamba mmoja alifariki dunia hospitalini hapo akiwa anapatiwa matibabu.

Alimtaja aliyefariki kuwa ni Regna Petro (14) ambaye ni mwanafunzi Shule ya Msingi Nyarulanga, kutokana na kuvuja damu nyingi baada ya kupata majeraha makubwa ya risasi tumboni. Aliwataja majeruhi wa tukio hilo kuwa ni Grace Malulu (11) mwanafunzi wa darasa la pili, Stanford Chubwa (48) ambaye alijeruhiwa vibaya usoni baada ya risasi kutoboa jicho lake moja na Edna Johachim aliyepatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

No comments:

Post a Comment