TSHISHIMBI.
LICHA ya kiwango kizuri alichokionyesha katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliofanyika dhidi ya Simba, kiungo mpya wa Yanga, Kabamba Tshishimbi, amesema kuwa bado hajaonyesha kiwango chake halisi cha uchezaji.
Tshishimbi juzi alionyesha kiwango cha juu katika mechi hiyo ya Ngao ya Jamii licha ya Yanga kupoteza mchezo huo na kuwafanya baadhi ya mashabiki wa timu hiyo kuondoka uwanjani na jina la nyota huyo mdomoni kutokana na kazi nzuri aliyoifanya.
Akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Tshishimbi, alisema kuwa amefurahi kuona mashabiki wa Yanga wakimpokea vizuri na kuliimba jina lake uwanjani.
“Sidhani kama nimecheza kwenye kiwango changu cha juu, unajua bado ni mgeni kwenye timu, baada ya muda na kuzoeana vizuri na wenzangu mashabiki wataona kiwango changu kilivyo,” alisema Tshishimbi ambaye mara baada ya mchezo huo alikuwa akilindwa na ‘makomandoo’ wa Yanga.
Aidha, alisema kuwa anawashukuru mashabiki kwa sapoti waliyoonyesha uwanjani wakati wa mchezo huo ambao walifungwa kwa penalti 5-4 baada ya kumaliza dakika 90 za kawaida bila kufungana.
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa nyota huyo wa mashindano tangu alipojiunga na Yanga siku chache zilizopita akitokea kwenye timu ya Mbabane Swallows ya Swaziland.
Kwa mara ya kwanza Yanga walimuona mchezaji huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akiwa na timu yake hiyo wakati ilipokuja nchini kucheza mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Azam FC.
No comments:
Post a Comment