KIUNGO WA SIMBA HARUNA NIYONZIMA AKIWA NA MSEMAJI WA TIMU HIYO HAJI MANARA.
KIUNGO wa Simba Haruna Niyonzima, amemsifu kiungo mpya wa Yanga, Kabamba Tshishimbi kwa kuanza vizuri kuitumikia klabu hiyo kutokana na kiwango alichokionyesha kwenye mchezo wa juzi wa Ngao ya Jamii.
Akizungumza na gazeti hili jana, Niyonzima, alisema kuwa ni ngumu mchezaji mgeni kufanya vizuri kwenye mchezo wa kwanza ambao unawakutanisha Simba na Yanga.
“Kwangu mimi naweza kusema ni mchezaji mzuri, ameanza vizuri, ameweza kukabiliana na presha ya mchezo huu, mchezo wa Simba na Yanga ni mgumu, lakini yeye ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga waliocheza vizuri,” alisema Niyonzima.
Kiungo huyo aliyesajiliwa na Yanga kutoka kwenye klabu ya Mbabane Swallows ya Swaziland, juzi alionyesha kiwango kikubwa na kuisaidia timu yake kumaliza dakika 90 huku wakiwa wamelingana nguvu na Simba kabla ya kuangukia pua kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti.
Simba iliendeleza ubabae linapokuja suala la upigaji panalti wanapokabiliana na Yanga baada ya kushinda kwa mikwaju 5-4 na kutwaa Ngao ya Jamii.
Hata hivyo katika hatua nyingine, Shirikisho la soka Tanzania (TFF) limeitaka klabu ya Simba kurejesha Ngao hiyo, ili ikafanyiwe marekebisho kutokana na kukosewa kuandikwa maneno yake.
TFF imeomba radhi kutokana na makosa hayo na huku pia, ikielezwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wake waliohusika.
No comments:
Post a Comment