Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeagizwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kuwakamata viongozi wa Chama cha Wakulima (TASO) Kanda ya Mashariki.
Viongozi hao wametakiwa kukamatwa ili kujibu tuhuma za ubadhirifu unaodiwa kufanyika, ikiwamo uuzaji wa ardhi kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere vya maonyesho ya siku kuu ya wakulima, Nanenane.
Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Wanawake, Watoto na Wazee, Dk. Hamis Kigwangala, kwenye kilele cha maadhimisho ya sherehe hizo kikanda.
Dk. Kigwangala ambaye alimuwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema imebainika uwepo wa majengo ambayo yanatumika kama makazi ya watu kwenye viwanja hivyo ambao wamedai kuuziwa viwanja na uongozi wa TASO.
Alisema ni vema viongozi wa TASO wakakamatwa ili kujieleza waliuza ardhi hiyo kwa kiasi gani, na fedha hiyo waliifanyia nini au ipo wapi.
Alisema TASO ilitakiwa kutambua kuwa mali za taasisi binafsi hubaki kuwa mali ya umma au kufilisiwa pindi zinaposhindwa kujiendesha.
"Msihangaike kutoa notisi sijui ya miezi mitatu (sijui) haitasaidia," alisema Dk. Kigwangala.
"La muhimu ndiyo hilo la kukamatwa na wajieleze na katika hili adhabu ni lazima itoke na iwe ya mfano kwa wengine wenye tabia kama hizi.”
Alisema kuwa eneo lote la uwanja limetengwa kwa ajili ya maonesho ya kilimo, uvuvi na mifugo na kwamba kuwauzia watu kufanya makazi ni kwenda kinyume na mipango ya eneo husika.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe aliiomba Serikali kuendelea kutilia mkazo mikoa kusimamia maonyesho hayo kufuatia makusanyo kuonekana milangoni kwa sasa tofauti na yalipokuwa chini ya TASO.
Dk. Kebwe alisema kuwa mwaka jana TASO ilikusanya Sh. milioni 75 katika maonesho yote huku yakiwa chini ya Tamisemi mwaka huu, kiasi cha Sh. milioni 175 kilikuwa kimepatikana mpaka juzi.
Hivyo, alisema Dk. Kebwe, kunaonekana kulikuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha katika maonesho hayo wakati wa uongozi wa TASO.
No comments:
Post a Comment