Siyo wabunge tu, bali hata baadhi ya watumishi wa Bunge nao wanadai kutowekewa mishahara yao ya mwezi uliopita.
Posho hizo za wabunge ni zile za majimbo ambazo huunganishwa katika mishahara yao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi alikiri kutowekewa fedha hizo kwa miezi miwili na si mwezi mmoja kama wabunge wengine wanavyodai.
“Sijawekewa kwa muda wa miezi miwili, sijui tatizo ni nini? Hata hivyo sijaamua kufuatilia kwa sababu nipo ‘busy’ na shughuli za jimboni kwangu.
“Baadhi ya wabunge wenzangu wanaogopa kusema ukweli, lakini hii ndiyo hali halisi ya Bunge letu. Kwani ukisema ukweli utashughulikiwa kama hawajaweka, hawajaweka tu ila wataweka,” alisema Mbilinyi maarufu kama Sugu.
Wakati Sugu akisema hayo, Mbunge wa Wawi (CUF), Ahmed Juma Ngwali alisema ameshawekewa fedha hizo na amethibitisha kwa kuangalia katika akaunti yake.
Mbunge mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema ; “Hadi juzi niliangalia katika akaunti sikuona kitu, lakini sijui sababu ni nini huenda utofauti wa akaunti za benki. Ila nakushauri watu wa kulisemea hili ni wahasibu wa Bunge,” alisema mbunge huyo.
Wakati hayo yakiendelea, Kaimu Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi alisema hakuna mbunge asiyewekewa fedha hizo, zote zimeshapelekwa benki pamoja na za watumishi wa chombo hicho cha kutunga sheria.
“Nimezungumza na wahasibu wamenithibitishia hili. Nadhani kutakuwa na tatizo katika benki husika, lakini walishaingiziwa stahiki zao. Nawashauri wabunge waangalie vema taarifa za akaunti zao ili kujiridhisha,” alisema Mwihambi.
Hata hivyo, taarifa zinaonyesha kuwa wabunge wameshalipwa mishahara tu, huku posho za jimbo zinazotumika kuwalipa wasaidizi wao wa majimboni zikiwa bado.
“Tumelipwa mshahara tu, fedha za jimboni ambazo zinatumika kulipa mishahara ya wasaidizi wetu hatujapata,” alisema mmoja wa wabunge wa Kanda ya Kusini.
Alisema hali hiyo imewafanya wengi wao kushindwa kufanya shughuli zao majimboni wakati mkutano mwingine wa Bunge ukikaribia kuanza.
Mbunge mwingine wa Kanda ya Ziwa, alisema kuchelewa kulipwa kwa posho hizo kumewafanya watafute utaratibu mwingine wa kuwalipa mishahara watu wanaowasaidia majimboni.
Alisema hata posho ya mwisho wa wiki kabla ya Bunge la Bajeti kumalizika, hawajalipwa hadi sasa ikiwa ni karibu mwezi mmoja baada ya kumalizika mkutano wa bajeti.
Wakati wa kuhitimisha Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuhakikisha wanatoa fedha kwa taasisi hiyo.
Aprili mwaka huu, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alieleza juu ya upungufu wa fedha unaolikabili Bunge na kwamba, vikao vya bajeti vingeshindwa kuendelea kama wasingetoa fedha.
Alisema awali walikuwa hawajapelekewa Sh8.3 bilioni kama bakaa ya bajeti ya mwaka 2016/17, lakini ili kukamilisha shughuli za mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, walitakiwa kukiongezea chombo hicho Sh21.1 bilioni.
Bajeti ya mwaka mzima ya Bunge ni Sh121.1 bilioni zilizoidhinishwa kwa Mwaka mpya wa fedha 2017/18.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment