KOCHA WA YANGA, MZAMBIA GEORGE LWANDAMINA.
Pamoja na ushindi huo, Yanga haikuonekana kucheza kwenye kiwango cha juu na kujikuta Singida United ikitawala kwa dakika nyingi kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa.
Akizungumza na Nipashe jana, Lwandamina alisema wachezaji wake walikuwa wazito kutokana na mazoezi magumu, lakini akawatoa hofu mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuwa mambo yatakaa sawa.
“Tulikuwa kwenye mazoezi ya ‘pre-season’ (kujiandaa na msimu mpya), yalikuwa magumu na wachezaji miili yao imekuwa migumu, lakini hii inatokea kwa timu nyingi wakati wa maandalizi ya msimu mpya baada ya michezo miwili watarudi kwenye kasi yao,” alisema Lwandamina.
Alisema mchezo huo wa juzi ulikuwa kwa ajili ya kuangalia yale aliyoyatoa kwenye mazoezi mkoani Morogoro kama yamewaingia wachezaji wake.
“Kwangu naona kambi yetu pamoja na mandalizi yetu kwa ujumla yamefanikiwa, tumekuwa na kikosi imara kwa sasa namalizia sehemu ya programu yangu kabla ya kuanza kwa ligi,” aliongeza kusema Lwandamina.
Aidha, alisema mashabiki wasiwe na hofu kwa kuwa timu yake imekamilika na usajili walioufanya ni wa mafanikio zaidi.
AWATEMA MNIGERIA, MCAMEROON
Katika hatua nyingine, imeelezwa wachezaji waliokuwa wakifanya majaribio kwenye timu hiyo, Mnigeria Henry Okoh na Mcameroon Fernando Bongyang wameshindwa kuonyesha viwango, hivyo hawatasajiliwa na timu hiyo huku dirisha la usajili likifungwa usiku wa kuamkia leo.
Mmmoja wa viongozi wa klabu hiyo aliliambia Nipashe kuwa wachezaji hao wameshindwa kulishawishi benchi la ufundi kuwasajili kutokana na viwango vyao.
“Hakuna ambaye atasajiliwa, hawajaonyesha uwezo na hawana kitu tofauti na wachezaji wetu wazawa, wote wameambiwa hakuna nafasi kwao,” alisema kiongozi huyo.
Wachezaji hao waliingia kipidi cha pili kwenye mchezo wa juzi wa kirafiki dhidi ya Sinigida United, lakini hawakuonyesha kiwango kizuri hususan Okoh aliyekuwa amevaa jezi namba tisa mgongoni na kuchezeshwa beki namba tatu.
Wachezaji hao walikuwa wakiwania nafasi moja kutimiza idadi ya wachezaji saba wa kigeni kwenye timu hiyo.
No comments:
Post a Comment