Tuesday, July 25, 2017

WAZIRI WA AFYA ATAKA WAGANGA WA TIBA ASILIA WASIWEKEWE VIKWAZO


Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kutowawekea vikwazo wataalamu wa tiba asili na mbadala ili waweze kujisajili na kutambulika kisheria.

Mwalimu ameyasama hayo jana  Jumatatu Julai 24 wakati akizindua Mpango Mkakati wa Tiba Asilia na Tiba Mbadala utakaoanza kutumika mwaka 2017 hadi mwaka 2022.

Alisema si lengo la Serikali kukandamiza au kuzuia tiba asilia bali inataka kuhakikisha dawa zinazotumika ni salama kwa afya za watumiaji.

“Ili kujua kama dawa ni salama lazima wajisajili, dawa zao ziangaliwe na inapothibitika kuwa ni salama basi zitumike, tusiwawakee vikwazo, ni wajibu wetu kuwawekea mazingira wezeshi kufikia hatua hiyo,”alisema.

Alisema zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanatumia tiba mbadala na asilia hivyo ni muhimu kuwepo uangalizi wa kutosha kuhakikisha dawa hizo hazileti madhara kwenye jamii.

Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Dk Edmund Kayombo alisema watalaamu 16,200 pekee ndio wamesajiliwa kisheria kutoa tiba hizo.

“Tunawahamasisha waje kujisajili, wapo wanaojitokeza ila wengi wao wanakwepa kwasababu hawataki kuonyesha miti wanayotumia,”alisema.

No comments:

Post a Comment