Mabingwa wa Kombe la SportPesa, Gor Mahia kutoka Kenya wanatarajia kuikaribisha Everton FC inayoshiriki Ligi Kuu England katika mechi ya kirafiki itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam-
huku mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney akisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka wa Tanzania.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, jana aliongoza viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa soka nchini waliojitokeza kuipokea timu hiyo ambayo imekuja nchini kwa mwaliko wa Kampuni ya SportPesa Tanzania.
Mechi ya leo itakuwa ni ya kwanza kwa Rooney tangu arejee katika klabu yake hiyo akitokea Manchester United ambayo aliitumikia kwa miaka 13.
Kocha wa Everton, Ronald Koeman, alisema kuwa kila mchezaji wa timu hiyo ambaye amekuja nchini atapata muda wa kucheza kuanzia dakika 45 na wataondoka kesho.
"Hii ndiyo mechi ya kwanza ya kirafiki na kila mchezaji nitampatia dakika 45. Tunacheza mpira kwa ajili ya kushindana, tunatarajia kupata ushindi katika mchezo huu utakaofanyika Tanzania," alisema.
Kocha Mkuu wa Gor Mahia, Dylan Kerr, alisema jana kuwa timu yake imejipanga kuitumia vizuri nafasi ya kucheza na Everton ambayo ina wachezaji wanaoshiriki moja ya ligi zenye kiwango cha juu duniani.
“Ninatumaini tutatumia vizuri nafasi hii kama ambavyo tulionyesha uwezo wetu na kuibuka washindi katika mashindano ya Kombe la SportPesa, hakuna timu ndogo katika dunia ya sasa, mpira ni uwanjani na si jina au taifa la mchezaji linalohusika kwenye mchezo,” alisema Kerr, kocha wa zamani wa Simba.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema jana kuwa maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na waamuzi wa hapa nchini wakiongozwa na Israel Nkongo, Fredinand Chacha na Frank Komba ambao wana beji zinazotambulika na Fifa ndiyo watachezesha mechi hiyo.
Alimtaja Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ndiye atakuwa mgeni rasmi katika mechi hiyo inayotarajiwa kuanza saa 11:00 jioni
huku kiingilio cha chini kikiwa ni Sh. 3,000.
No comments:
Post a Comment