DENI la serikali kwa Bohari ya Dawa (MSD) limebaki Sh. bilioni 47 baada ya kulipa Sh. bilioni 96 katika Sh. bilioni 143 ilizokuwa ikidaiwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa MSD, Sako Mwakalobo, aliieleza Nipashe katika mahojiano maalum kuwa awali serikali ililipa Sh. bilioni 11.4 na mwaka huu zimetengwa Sh. bilioni 85.
Alisema fedha hizo ni lazima zitalipwa ili kuipa MSD uwezo wa kununua dawa kutoka viwandani.
"Hatuna madeni yoyote na wazabuni wetu, yaliyopo ni ya kawaida ya mchakato wa manunuzi ambao ni siku 30 au 60," alisema Mwakalobo. "Hatuna ugomvi nao (wazabuni) tunaweza kusalimiana."
Alisema ununuzi wa dawa moja kwa moja kutoka viwandani umesaidia kuongeza upatikanaji na kupungua kwa bei.
Faida nyingine, alisema Mwakalobo, ni kuokoa gharama na uhakika wa ubora wa dawa hizo kwa kuwa hakuna mtu wa kati.
Aidha, Mwakalobo alisema kuongezeka kwa uwezo wa kifedha wa MSD baada ya kulipwa deni la serikali kuna uwezekano mkubwa wa kuongeza viwanda vya uzalishaji nchini kwa kuwa wazalishaji watakuwa wameona fursa za uwekezaji kutokana na imani ya malipo inayojengwa sasa.
"Tukiwa na viwanda vingi itapunguza kutumia fedha za kigeni kwa ajili ya kununua dawa nje," alisema.
Mwakalobo alisema kuna maduka ya dawa saba nchini yanayomilikiwa na MSD, ambayo yalianza Desemba 2010.
Aliyataja maduka hayo kuwa ni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali za mikoa ya Mbeya, Sekoture (Mwanza) na Mount Meru (Arusha), Hospitali za wilaya za Chato, Ruangwa na Katavi.
"Lengo la kuanzisha maduka ni kusogeza huduma karibu na wananchi, hususani kwenye hospitali, ili kufanya dawa ambazo hazipatikani kwenye mfumo wa kawaida wa MSD zipatikane kirahisi," alisema Mwakalobo.
Hata hivyo, Mwakalobo alisema "nia ya MSD siyo kuendelea na maduka."
"(Nia ya MDS) ni kuhakikisha hospitali, halmashauri na vituo vya afya vinachukua jukumu la kuanzisha maduka yao nasi tutawapa wataalamu na dawa.
"Tungependa fedha inayopatikana isaidie hospitali na vituo vya afya."
Alisema kwa sasa hospitali nyingi zimeomba msaada wa kufunguliwa maduka, na kwamba wengi wananunua dawa MSD ili kuhakikisha wagonjwa hawatoki nje ya hospitali kutafuta dawa.
"Haya maduka mwaka jana yametulea zaidi ya Sh. bilioni 5, hivyo gharama za maduka zinaweza kulipwa na mauzo. Tutaendelea kuyaimarisha kuwe na dawa za kutosha," alisema.
Mwakalobo alibainisha, hata hivyo, changamoto kubwa ni gharama za uendeshaji kwa kuwa Sheria ya Famasia inataka duka liwe na mtaalamu wa kuliendesha jambo linaloongeza gharama.
"Maduka wakati yanaanzishwa ilikuwa ni kuuzia wateja ambao ni hospitali, lakini yanavyofanya kazi ni tofauti na malengo kwa kuwa wanauza dawa moja kwa moja kwa wateja kwa kuwa hospitali hawanunui kutoka kwenye maduka hayo," alisema.
Mwakalobo pia aliiambia Nipashe kuwa ongezeko kubwa la uwezo wa kifedha wa MSD kutokana na kuongezeka kwa bajeti ya serikali katika mwaka wa fedha wa 2017-2018 umeiwezesha kuaminiwa na wazalishaji wa dawa wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, alisema ongezeko hilo la uwezo wa kifedha limefanya MSD iwezeshe upatikanaji wa dawa nchini kuwa wa hakika kwa asilimia 83 na kutaraji uwe asilimia 90 ifikapo Desemba, mwaka huu.
Alisema kiasi cha fedha katika bajeti ya MSD kilipanda kutoka Sh. bilioni 30 mwaka uliotangulia 2016-2017 hadi Sh. bilioni 251 mwaka jana na kwamba thamani ya fedha hizo ilipanda zaidi kufuatia maelekezo ya Serikali ya kununua dawa moja kwa moja kutoka viwandani.
Kwa mwaka wa fedha wa 2017-18, Mwakalobo alisema zaidi, Serikali imeongeza bajeti hadi kufikia Sh. bilioni 269.
"Uhaba wa fedha ulisababisha MSD kushindwa kununua dawa, kuwalipa wazabuni na dawa kupanda bei kwa kuwa wengi hawakujua watalipwa lini licha ya kutoa huduma," alisema Mwakalobo kwa kuwa "asilimia 80 hadi 90 ya dawa zinaagizwa kutoka nje."
Alisema serikali ya awamu ya tano baada ya kuingia madarakani iliweka kipaumbele kwenye ununuzi wa dawa moja kwa moja kutoka viwandani, jambo ambalo lilishindikana awali kwa kuwa MSD haikuwa na fedha.
"Unaponunua moja kwa moja kwa mzalishaji lazima kifurushi (fedha) kiwe cha kutosha," alisema Mwakalobo.
"(Lakini) kwa uwezo wa kibajeti tuliopewa sasa, wa kuongezwa kwa takribani mara 800, na fedha imeletwa kama ilivyopangwa kila mwezi na hadi mwisho wa mwaka hakuna fedha ambayo haijaletwa, tuna uhakika wa dawa."
No comments:
Post a Comment