Rais John Magufuli anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi mkoani Singida leo Julai 25 ambapo pia atazindua barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya yenye urefu wa Kilomita 89.3.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Jumatatu Julai 24, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi amesema Rais Magufuli anatarajiwa kufanya uzinduzi wa barabara hiyo katika eneo la NjiaPanda, Itigi na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.
“Napenda kuwataarifu wananchi wote kuwa rais wetu mpendwa atatuzindulia barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya, hivyo basi tujitokeze tukamshukuru kwa kutuletea maendeleo wana Singida, ametufanyia jambo kubwa sana, shukrani zetu hiyo leo pale njiapanda zitaendelea kumpa hamasa ya kutuletea maendeleo zaidi,” amesema Dk Nchimbi.
Dk Nchimbi ameongeza kuwa wananchi wajitokeze kumlaki na kutoa pongezi kwa Rais Magufuli kwa kuokoa rasilimali za nchi hasa katika sekta ya madini.
“Rais Magufuli ameokoa rasilimali nyingi za taifa na anapambana usiku na mchana kuzilinda ili Watanzania hasa wanyonge wafaidike, wengi tumekuwa tukifurahishwa sana na jitihata hizo, hivyo basi kesho tuonyeshe upendo wetu na shukrani zetu kwake,” ameongeza Dkt Nchimbi.
Pia amesema barabara itakayozinduliwa leo na Rais Magufuli ni kiunganishi muhimu kati ya Mkoa wa Singida na Tabora na hivyo kurahisIsha usafirishaji tofauti na ilivyokuwa kabla ya kujengwa.
Barabara hiyo pia itawarahisishia safari wasafiri wa mikoa ya Singida na maeneo ya jirani kuelekea mkoa wa Tabora mpaka Kigoma.
No comments:
Post a Comment