Wednesday, June 14, 2017

HII KALI:MJADALA WA KATIBA MPYA WAIBUKA BUNGENI


Wakati Wabunge wakijadili hoja kuhusu kusiaiwa mikataba mibuvu ya Madini hoja ya katiba mpya iliibuka kwa wabunge kadhaa waliosimama kuchangia walipaza sauti zao wakidai kuwa tatizo linaanza kwenye Katiba.

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), ndiye alikuwa wa kwanza kutoa hoja hiyo wakati akichangia makadirio ya bajeti ya mwaka 2017/2018.

Alisema wizi huo ulioisababishia serikali kukosa mapato ya matrilioni ya fedha ulifanyika Mkapa na Kikwete wakiwa madarakani hivyo lazima mabadiliko ya Katiba yafanyike ili wahojiwe na kufikishwa mahakamani.

“Mheshimiwa Spika kama kweli Rais John Magufuli yuko serious (thabiti) na suala hili alete mabadiliko ya Katiba hapa bungeni ili tuwaondolee kinga hawa marais wastaafu wahojiwe na washtakiwe, maana haya yote yalifanyika wakiwa madarakani,” alisema Heche.

Alisema maamuzi yote yaliyotiliwa shaka na kamati yaliyofanywa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati wa Mkapa, Daniel Yona na mawaziri waliomfuatia yalipata baraka za wakuu wao, hivyo kama watahojiwa kwa makosa waliyofanya lazima na marais hao wakamatwe na kuhojiwa.

Kwa mujibu wa kamati maalumu ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na makinikia yanayosafirishwa nje ya nchi iliyowasilishwa Ikulu jijini Dar es salam juzi, nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka sh. trilioni 489 katika miaka 19 iliyopita.

Kamati hiyo iliundwa na Rais John Magufuli Aprili 10 ikiwa na wajumbe nane wabobezi katika sheria na uchumi, na mwenyekiti wake Profesa Nehemia Osoro alisema kwa kima cha chini, nchi imepoteza sh. trilioni 252 katika kodi na mali (thamani ya madini) yaliyotoroshwa kupitia makinikia.

Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema), naye alipendekeza marais wastaafu waondolewe kinga kupitia mabadiliko ya Katiba ili wahojiwe na kufikishwa mahakamani kutokana na wizi uliofanyika kwenye sekta ya madini.

Lijualikali aliyekaa gereza la Ukonga kwa miezi miwili mwanzoni mwa mwaka kabla ya kushinda rufani ya kifungo cha miezi sita, alisema haitakuwa sahihi kuwakamata na kuwafikisha mahakamani mawaziri na viongozi mbalimbali waliohusika kwenye kadhia hiyo na kuwaacha marais wastaafu ambao wakati hayo yanafanyika walikuwa wanaona.

“Haiwezekani na wala si haki mtu kama Adrew Chenge (Mwanasheria Mkuu wa zamani) ahojiwe halafu rais ambaye alikuwa bosi wake aachwe," alisema Lijualikali.

"Akina Nazir Karamagi (Waziri wa Nishati wa zamani) hawakuwa na uwezo wa kufanya mambo waliyofanya bila viongozi wao kujua... kwa hiyo nawaomba wabunge wenzangu hii vita iwe ya wote.

"Pia CCM na serikali yenu mnapaswa kuwaomba radhi Watanzania kwa wizi huu.”

Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), alipendekeza marais hao wastaafu waondolewe kinga ya kutokushtakiwa ili nao wahojiwe kama wana makosa kwenye sakata la wizi kwenye sekta ya madini.

“Mheshimiwa Spika kama mawaziri walifanya makosa basi marais wastaafu walijua kwasababu mambo haya yanafanywa kwa uwajibikaji wa pamoja; hivyo uletwe muswada wa mabadiliko ya Katiba tuwaondolee kinga nao washtakiwe,” alisema Msigwa.

Kamati hiyo ya watu nane iliyokuwa chini ya Prof Osoro ilitoa mapendekezo 21 ambayo Rais alisema ameyakubali yote kwa asilimia 100.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni Serikali kufanya uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliokuwa Mawaziri, Wanasheria Wakuu wa Serikali na Manaibu wao kwa kipindi chote cha utoroshaji madini huo.

Wengine wa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa ripoti hiyo ni Wakurugenzi wa idara za mikataba, na Makamishna wa madini, wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini.

Wengine ni watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni.

Wengine ni watumishi na wamiliki wa makampuni ya madini, makampuni yaliyohusika kuandaa nyaraka za usafirishaji wa makinikia(Freight Forwarders(T)Ltd na makampuni ya upimaji wa madini kwa kuvunja sheria za nchi na upotoshaji.

No comments:

Post a Comment