Gari la Polisi
Mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda waliyokuwa wakitumia kusafiri, kugongana uso kwa uso na gari la Jeshi la Polisi katika wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Ajali hiyo ni ya juzi saa 9:30 alasiri katika kijiji cha Sokolaboro, ikilihusisha gari la polisi lenye namba za usajili PT 1893 aina ya Toyota Land Cruiser, lililokuwa likiendeshwa na askari aliyetajwa kwa jina la Konstebo Mohamed.
Aliyekufa katika ajali hiyo ni mkazi wa Kijiji cha Omoche wilayani Rorya, Keraryo Paulus (27), aliyekuwa akiendesha pikipiki hiyo yenye namba za usajili MC 745 ACD. Abiria wa bodaboda hiyo aliyejeruhiwa ni mkazi wa Kijiji cha Masike wilayani Rorya, Festo Chobe (40), ambaye amelazwa kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya Shirati wilayani humo.
Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Sweetbert Njewike, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo katika mazungumzo na HabariLeo kwa njia ya simu jana. Alifafanua kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa bodaboda, aliyeyumba barabarani upande wa kushoto kisha kugongana na gari hilo.
Hata hivyo, Kamanda Njewike alikanusha tuhuma kwamba dereva wa gari la polisi, Konstebo Mohamed, hana leseni na usajili wa kuendesha gari hilo. Kadhalika, alikanusha taarifa kwamba Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Rorya, William Mlowola, alimwondoa dereva halisi wa gari hilo aliyetajwa kwa jina la Andrew na kulikabidhi Konstebo Mohamed.
No comments:
Post a Comment