Wednesday, May 17, 2017

VIONGOZI WA SIMBA WAKUTANA NA MOHAMMED DEWJI

Mfanyabiashara bilionea kijana Mohammed Dewji.

Uongozi wa Simba, jana ulitarajia kukutana na Mohammed Dewji maarufu kama MO, aliyeamua kujitoa katika suala la mchakato wa mabadiliko ya klabu hiyo kufuatia uongozi huo kuingia mkataba na Kampuni ya Mchezo wa Kubashiri ya SportPesa.

Hali hiyo ilionekana kumkasirisha MO kutokana na uongozi wa klabu hiyo kutomshirikisha licha ya kuwa na makubaliano naye ya kimkataba kwa baadhi ya mambo ya ndani ya klabu hiyo. Kutokana na hali hiyo, MO aliamua kujiweka pembeni na klabu hiyo lakini pia akiutaka uongozi huo umlipe gharama zake kiasi cha Sh bilioni 1.4 alizokuwa akizitoa kwa ajili ya malipo ya mishahara ya wachezaji wa timu hiyo.

Akizungumza na Championi Jumatano mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu kabisa ya Simba ambaye aliomba kutotajwa jina lake alisema kuwa jana usiku walikuwa wakutane na MO kwa ajili ya kumaliza tofauti zao hizo ikiwa ni pamoja na kumuomba msamaha kwa yote yaliyotokea.

“Tunatarajia kukutana na MO leo hii usiku (jana), kwa ajili ya kuzimaliza tofauti hizi zilizojitokeza hivi karibuni kwani kusema kweli baada ya kukaa na kutafakari tuliona hatukumtendea haki.

“Hata hivyo nisingependa utaje jina katika habari yako hiyo kama mimi ndiye niliyekuambia kwa sababu tunataka kulifanya jambo hili kwa siri kidogo,” alisema kiongozi huyo na kuongeza kuwa.

“Katika mkutano huo pia tutajadiliana na kuhusiana na mikataba ya baadhi ya wachezaji wetu akiwemo Ibrahimu Ajibu pamoja na Jonas Mkude ambao mara kwa mara wamekuwa wakihusishwa kutaka kuondoka. “Baada ya kikao hicho tutawajulisha wanachama wetu nini kilichoendelea kati yetu na MO lakini pia wachezaji hao,” alisema kiongozi huyo.

No comments:

Post a Comment