Wednesday, May 3, 2017

SPIKA AZIWEKA REHANI AJIRA ZA WATUMISHI BUNGENI

SPIKA WA BUNGE, JOB NDUGAI.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, ametishia kuwafukuza kazi watumishi wanne wa Bunge wanaofanya kazi kwenye ofisi za Kambi Rasmi ya Upinzani ikiwa wataendelea kuandika hotuba alizoziita zenye maneno machafu dhidi ya uongozi wa Bunge.

Aliyasema hayo bungeni jana wabunge walipoazimia kuwasamehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema) waliokutwa na hatia ya kukidharau chombo hicho cha kutunga sheria.

Ndugai mbali na kuipongeza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kazi nzuri ya kuwahoji viongozi hao waliolalakiwa, alisema amebaini kuna ‘mchezo mchafu’ dhidi ya uongozi wa Bunge unaofanywa na wanaoandika hotuba za upinzani.

Alisema hotuba kadhaa za upinzani zimekuwa na maneno yanayoashiria kudharau Bunge, hasa Kiti cha Spika.

“Nimefanya utafiti wangu. Kwa mfano, siku moja alisoma hotuba Ruth Mollel (Waziri Kivuli, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), namfahamu yale maneno yaliyokuwa yameandikwa kule najua kabisa Ruth hawezi kuyaandika, kuna mtu anaandika, nilimwambia siku ile,” Ndugai alisema.

“Kwa hiyo, nikafanya utafiti wangu katika Ofisi ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kuna vijana wanne; Onesful Mbuya, Olivia Mwikira, Jonathan Wilfred na Dorice Konela, hawa waliombewa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni wanahitaji kuongeza nguvu ya kufanya utafiti na mambo mbalimbali kuhusu taarifa zinazosomwa.

“Sasa hawa tunawalipa sisi, yaani kwa maneno mengine nawalipa mimi halafu wanakaa na kuandika hotuba za kunituhumu mimi hapa. Mimi sijawahi kuona vitu vya namna hiyo na ninyi hamkai mkawaambia hawa watoto, siku hizi ajira hakuna.

Hivi unatuhumu mwajiri wako kizembezembe, uliona wapi kitu kama hicho duniani? alihoji.

Alisema ameshazungumza sana suala hilo na kwamba kuanzia sasa watachukua hatua na kuongeza kuwa vijana hao nao amewasamehe kwa sasa kama ambavyo Bunge lilifanya jana kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar na viongozi wengine waliofikishwa mbele ya Kamati ya Maadili.

Alisema kuanzia sasa atakayelituhumu Bunge, ataanza kumvaa bila kujali kama ni maoni ya kambi.

“Halafu huyu Spika unayejaribu kumdharau, baadhi yetu ni baba zao, mambo yakituendea mrama kivyovyote vile, utarudi kwake yeye. Ukiugua hapa, ukifanya nini hapa sasa unamtukana na kumdharau, naye akichukua moyo wako wewe,” alisisitiza.

“Kama alivyosema Rais (John) Magufuli kule Zanzibar, wewe unaleta za kuleta halafu mkono wangu huu uidhinishe kwenda India? Tujenge mahusiano, tufanye kazi bila chuki,” alisema.

Hata hivyo, Spika Ndugai alisema nia yake si kulifanya Bunge hilo kuwa kama kanisa au msikiti, bali watu watoe hoja zao wanavyoweza kwa lugha ya staha.

No comments:

Post a Comment