Wednesday, May 3, 2017

POLISI ALIYEMFYATULIA RISASI DEREVA WA BODABODA MATATANI


JESHI la polisi mkoani Tanga, limemfungulia jalada la uchunguzi askari wake aliyemjeruhi kwa risasi mwendesha bodaboda Isdory Justin (27) katika tukio lililotokea Barabara ya Nane na Taifa, jijini Tanga.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Benedict Wakulyamba, alisema tukio hilo lililotokea Aprili 27, mwaka huu, saa 2:38, wakati askari watano wakiwa doria ya kawaida katika eneo hilo.

Alisema siku ya tukio hilo, askari hao wakiwa katika doria, waliwakuta watu wengi hasa vijana wakiwa katika eneo hilo pamoja na mchoma mahindi, wamekusanyika na kwa utaratibu wa kawaida wa jeshi, waliwataka watu hao waondoke kwa kuwa ni usiku.

Kamanda Wakulyamba alisema baada ya polisi kuwataka waondoke, mchoma mahindi alitii na kufunga biashara yake na kuondoka na watu wengine, lakini alijitokeza mtu mmoja kuhoji hatua ya polisi kuwataka kuondoka akidai kwamba wanasubiri abiria, watakaoshushwa na mabasi.

Wakulyamba alisema askari hao waliwaeleza kwamba eneo hilo halikuwa na kituo cha basi hivyo waondoke, lakini mtu huyo alikuwa anabishana na askari huyo ndipo mmoja wa askari aliyekuwa ameshika bunduki, aliiweka sawa kwa lolote litakalotokea baada ya watu wengine waliokuwa wameondoka kurudi tena.

"Askari wengine walimdhibiti yule kinara wa ulalamikaji ili wamchukue kwenda naye kituoni na walipokuwa katika mita 50 hivi walipoondoka naye, yule kijana alitupa baiskeli yake aliyokuwa nayo na kumvamia yule askari aliyekuwa na bunduki ikasababisha ’magazini’ ya silaha ile kutoka eneo lake," alisema Kamanda huyo.

Alisema katika purukushani ile, risasi ilifyatuka na kumpiga kijana huyo wa bodaboda sehemu ya chini ya tumbo na kusababisha ajeruhiwe vibaya na polisi walimpeleka katika Hosptali ya Rufani ya Mkoa ya Bombo, ambako baadaye ndugu zake walimhamishia Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambako anapatiwa matibabu hadi sasa.

"Yule askari tunamshikilia na tumefungua jalada la uchunguzi kubaini ukweli wa tukio hilo ingawa wananchi haya ninayowaeleza ndiyo waliyosema. Tukipata ukweli kama askari wetu alifyatua kwa uzembe tutamchukulia hatua lakini kama yule kijana alikuwa na nia ovu ya kutaka kupora bunduki pia tutachukua hatua,” alisema.

Hata hivyo, kamanda Wakulyamba alitoa rai kwa wananchi kutii sheria bila shurti ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kama ilivyokuwa kwa tukio hilo ambalo lingeweza kuepukika endapo wale wangetii amri kwa kuondoka mahali hapo.

No comments:

Post a Comment