Rais
John Magufuli ametangaza kuwa Serikali yake itatoa nyongeza ya mshahara
ya mwaka na kupandisha madaraja ya kazi kuanzia Bajeti ya mwaka ujao wa
fedha 2017/18.
Aidha,
amepiga marufuku wafanyakazi wa Serikali kuhamishwa kituo cha kazi bila
kulipwa stahiki zake, akisema lengo la hatua hiyo ni kuepusha madai
yasiyo na sababu.
Rais Magufuli alisema hayo jana kwenye sherehe za Sikukuu ya Mei Mosi zilizofanyika kitaifa Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema
Serikali ililazimika kufanya ukaguzi wa watumishi wake wote kabla ya
kufanya uamuzi wowote kuhusu maslahi ya wafanyakazi na kwamba baada ya
kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi atakaa na Baraza la
Mawaziri kufanya maboresho.
“Acheni
tufagie nyumba kwanza, mlitaka nitangaze nyongeza huku wakiwamo
watumishi hewa na wasio na vyeti? … Mwaka huu tutapandisha madaraja ya
kazi na kuweka nyongeza ya mishahara kuwa sawa na madaraja stahiki
ambayo yapo kisheria,” alisema.
Rais
alisema mchakato wa kusafisha watumishi wenye upungufu na hewa ulikuwa
mgumu, hivyo ni wakati mwafaka kwa ambao wanastahiki kupata promosheni
kunufaika, kwani wangefanya kabla kundi la wafanyakazi 19,000
waliondolewa lingekuwapo.
Magufuli
alisema pamoja na kuongeza mishahara na kupandisha vyeo, Serikali
inatarajia kuajiri zaidi ya wafanyakazi 52,000 ili kuziba mapengo
mbalimbali katika utumishi wa umma.
“Mei
Mosi si kwa ajili ya Tanzania bali duniani kote. Ni siku ya
kukumbushana na kutafakari mambo kuhusu wafanyakazi na kutatua matatizo
yanayowakabili, hivyo nimechukua changamoto zenu na ninaahidi kuzifanyia
kazi,” alisema.
Alipongeza
viongozi wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), kwa kutambua
dhamira ya Serikali, hivyo kuwaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano ili
kuchangia maendeleo ya Taifa.
Aidha,
alisema changamoto za kisheria zinazowakabili wafanyakazi, waziri
husika atazifikisha bungeni na zikipitishwa atasaini muda huo huo.
“Nawahakikishia
kuwa tunaanza ukurasa mpya. Ndiyo maana mnaona hii siku ni tofauti.
Serikali tumeamua kuimarisha maslahi ya wafanyakazi. Na nyie muwe tayari
kuchapa kazi,” alisema.
Rais
Magufuli alisema wafanyakazi ndio injini ya maendeleo katika Taifa
lolote kubwa duniani, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja kwa
maslahi ya nchi na wananchi.
Kuhusu
fao la kazi, alisema Serikali inalifanyia kazi na kuna mchakato
unaendelea mfanyakazi anapoacha ajira kabla ya kustaafu, alipwe sehemu
ya mafao.
Akizungumzia
bima, alisema Serikali inaendelea na utaratibu wa kuanzisha fao la Bima
ya Ajira na wadau wameshatoa maoni, hivyo wakati ukifika watapewa
taarifa rasmi.
Akijibu
hoja ya uhuru wa wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi, alisema
suala hilo lilishazungumzwa mwaka jana na lipo kwa mujibu wa sheria na
hakuna mwajiri aliye juu ya sheria.
Kwa
upande mwingine, Rais Magufuli ameziagiza wizara na taasisi kuunda
mabaraza ya wafanyakazi kulingana na mahitaji na kuwa kwa sasa yapo
mabaraza 478.
Aidha, alitaka waajiri kutoa mikataba ya ajira kwani ni jambo la kisheria na si hiari.
Akijibu
madai ya wafanyakazi baada ya kuhamishwa eneo la kazi, Rais aliwataka
wafanyakazi kutohama eneo bila kulipwa stahiki zao, kwani ni kinyume na
sheria.
Rais
Magufuli alisema hakuna sababu ya mfanyakazi kuhamishwa bila kulipwa,
kwani kinachoendelea ni lawama kwa Serikali, jambo ambalo hataki
kulisikia tena.
Aidha,
kuhusu mfumuko wa bei, Rais alisema Serikali ipo kwenye mkakati wa
kuhakikisha hali hiyo inadhibitika, huku akibainisha kuwa mvua
zinazoendelea kunyesha zitafanikisha mchakato huo.
Halikadhalika
Rais alisisitiza kuwa Serikali ina mpango wa kuboresha na kufufua
viwanda hali ambayo itachangia kuongezeka kwa ajira.
Alisema kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii jumla ya dola za Marekani milioni 156 zitatumika kujenga viwanda nchini.
No comments:
Post a Comment