Shirikisho
la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeitaka Serikali
kuharakisha mchakato wa fao la kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii
ili wafanyakazi wapate haki yao.
Limeitaka
pia kuangalia upya makato ya kodi ya mishahara ili yanufaishe watumishi
wote na kueleza kuwa kilichopunguzwa mwaka jana kinalinda wafanyakazi
wachache wa kima cha chini cha mishahara.
Katibu
Mkuu wa Tucta, Dk Yahya Msigwa, alisema hayo kwenye hotuba ya
Shirikisho hilo mbele ya Rais John Magufuli kwenye Maadhimisho ya Siku
ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika mjini Moshi, Kilimanjaro jana.
Alisema
kwa muda mrefu wafanyakazi wamekuwa wakisubiri upitishwaji wa fao hilo
ambalo litawasaidia kujikimu wanapokosa ajira huku akiongeza kuwa
kiwango cha kodi ya asilimia tisa kinachotozwa kinanufaisha watumishi wa
mshahara wa kima cha chini.
“Tunaiomba
Serikali iharakishe kuanzisha fao la kukosa ajira, ili linufaishe
wafanyakazi. Kingine vikokoteo vya mafao ya mifuko ya jamii viboreshwe
ili watumishi waone matunda ya kuchangia,” alisema Dk Msigwa.
Aliishauri
Serikali kufanya maboresho kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo
kuunda mifuko miwili wa umma na wa binafsi ili kuondoa mkanganyiko wa
vikokoteo uliopo, wingi wa mifuko ya hifadhi na kupunguza muda wa
wastaafu kusotea mafao.
Alifafanua,
kwamba baada ya Serikali kupunguza kiwango cha kodi ya mishahara (PAYE)
kutoka asilimia 11 hadi tisa, TUCTA imebaini wafanyakazi wanaopokea
mishahara ya kima cha chini ndio wanufaika wakubwa, huku wenye kima cha
juu wakiendelea kubanwa.
Kuhusu
wawekezaji, Dk Msigwa alisema wapo wanaokiuka sheria za kazi na kanuni
za ajira, ikiwamo kunyima wafanyakazi haki ya kuunda vyama vya kutetea
maslahi yao, pamoja ulipaji mishahara kibaguzi.
Alibainisha
kuwa wapo wawekezaji wanaolipa watumishi wenye Shahada kutoka nje ya
nchi Sh milioni saba na kuwalipa wazawa Sh 700,000.
Aidha,
aliiomba Serikali kuzifanyia maboresho sheria za utumishi wa umma
zinazohusu uhusiano wa kazi ili ziwawezeshe kupeleka masuala yao kwenye
Mahakama ya Usuluhishi ya Masuala ya Kazi (CMA).
Pia
aliitaka Serikali kuwezesha majaji kwenda mikoani kumaliza usikilizaji
kesi za wafanyakazi kwa wakati na haki itendeke huku akibainisha
kuipunguzia majukumu Wizara ya Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu ili
ishughulikie matatizo ya wafanyakazi.
Alisema
TUCTA inaipongeza Serikali kwa kupambana na rushwa, ufisadi, kuondoa
watumishi hewa, kupambana na dawa za kulevya na uboreshaji wa maslahi ya
wafanyakazi.
No comments:
Post a Comment