Monday, May 1, 2017

MBEZI,KIBAHA,TEMBONI KUONJA MAFANIKIO YA MRADI WA DAWASA


HUDUMA ya maji ni muhimili kwa maisha ya mwanadamu kwani ni moja ya mahitaji ambayo yakikosekana kabisa uhai wa binadamu na viumbe hai kwa ujumla wake huwa mashakani.

Pamoja na maji kuwa ni muhimu kwa shughuli za usafi wa mazingira pia husaidia jamii kukabiliana na tatizo la maradhi yatokanayo na ukosefu wa maji safi ikiwemo magonjwa ya matumbo, kuhara na kipindupindu. Kwa kutambua umuhimu wa maji kwa wananchi, Serikali imekuwa na mipango na mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wakiwemo wakazi wa Jiji mashuhuri la Dar es Salaam ambapo idadi yao imekuwa ikiongezeka siku hadi siku. Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) imekuwa ikibuni na kutekeleza miradi mikubwa ya kupunguza adha ya maji kwa wananchi wa jiji hilo na mkoa jirani wa Pwani ambao pia wanahudumiwa pia na mamlaka hiyo.

Moja ya miradi inayotekelezwa katika muktadha huo ni ule wa uboreshaji wa mfumo wa ugawaji na usambazaji maji katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo na Mbezi Luis hadi Kimara ili kuwezesha wananchi kupata maji ya kutosha. Hivyo mradi wa uboreshaji wa huduma ya majisafi kati ya eneo la Kibaha mkoani hadi Mbezi Temboni jijini Dar es Salaam utakuwa ni mkombozi kwa wananchi wa maeneo hayo ambayo walikuwa wakisubiri kwa hamu kukamilishwa mradi huo.

Wananchi wa Mbezi Temboni wanasema uamuzi huo wa kuwaletea mradi huo ni wazi kuwa umelenga kumaliza zama za matatizo ya maji na kwamba kwa sasa wataelekeza nguvu zao katika masuala mengine ya ujenzi wa Taifa, ikiwemo kuyatumia maji hayo pia katika shughuli za usafi wa mazingira na kuweza kujikinga na maradhi. Mmoja wa wananchi waliozungumza na mwandishi wa makala haya, Halima Pazi, anasema kwa miaka mingi wamekuwa wakipata maji kwa kusuasua kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwepo ikiwemo uchakavu wa miundombinu na maji mengi kuishia njiani .

Halima anaamini kwamba kwa ujio wa mradi huo ni wazi watakuwa wakipata maji mengi yatakayotosheleza mahitaji yao ya kibinadamu na kuyatumia katika shughuli nyingine za hifadhi ya mazingira na usafi kwa ujumla wake. Pazi anashukuru uamuzi wa Serikali wa kuwekeza katika miradi ya aina hiyo kwani ni dhahiri tatizo la maji litakuwa historia katika maeneo hayo na kuomba mradi huo ukamilishwe kwa wakati ili kuchochea kasi ya maendeleo ya jamii katika eneo hilo.

Akizungumzia mradi wa eneo la Kibaha Mkoani hadi Mbezi Luis Temboni, Mkurugenzi wa huduma za Ufundi wa Dawasa, Romanus Mwang’ingo anasema mradi huo utahusisha ujenzi wa mtandao wa majisafi katika maeneo yatakayohudumiwa na tangi la Kibamba lililo na uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo milioni 10. Pia anabainisha kuwa kwa upande wa kaskazini mwa tangi hilo, mfumo mpya utajengwa katika eneo la Luguruni ambapo upande wa mashariki mfumo utajengwa katika eneo la Mbezi Inn, Mbezi Temboni na Msigani huku upande wa Kusini mtandao utajengwa katika eneo la Kwembe na Magharibi mtandao utajengwa eneo la Kibamba, Kisarawe, Visiga, Kiluvya, Uyaoni na Mkoani.

Anasema mradi huo utahusisha ulazaji wa mabomba ya ugawaji maji ya chuma yenye ukubwa wa kati ya inchi 10 (DN250) na inchi 16 (DN400) kwa umbali wa kilometa 28 ikihusisha pia ubadilishaji na ukarabati wa mabomba yaliyokuwepo. Kazi hii itafanyika kuanzia Mbezi Temboni hadi Mkoani na Uyaoni. Pia kutafanyika ulazaji wa mabomba ya ugawaji maji mitaani ya mpira mgumu (HDPE) yaliyo na ukubwa wa kati ya inchi nane (DN200) na inchi tatu (DN 90) kwa umbali wa jumla ya kilometa 357 ndani ya eneo hilo lililopo kati ya Mbezi Temboni na Kibaha Mkoani.

“Kazi nyingine itakayofanyika ni ya ufungaji wa mita kubwa ya kupima wingi na msukumo wa maji yanayoingia mitaani na ufungaji wa valvu za kudhibiti msukumo wa maji katika maeneo mbalimbali,” anasema Mwang’ingo. Mhandisi huyo anasema pia kutafanyika kazi ya ufungaji wa maeneo 11 maalumu kwa ajili ya kuhudumia magari ya zimamoto, ukarabati wa matoleo (off take) katika bomba kuu, ukarabati wa maeneo ya ugawaji maji na kufanya maunganisho kati ya tangi jipya na mtandao wa maji uliopo. Pia utafanyika ufungaji wa mtambo wa kisasa wa kusoma mita (wireless telemetry meter reading) na ufungaji wa kifaa maalum cha kupokea taarifa za mita.

Kifaa hicho kitafungwa katika ofisi za Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) makao makuu. Ofisa Uhusiano na Jamii wa Dawasa, Mecktridis Mdaku anasema utekelezaji wa mradi huo wa uboreshaji wa huduma ya ugawaji maji katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, ulianza rasmi mwezi Machi mwaka 2016. Mdaku anasema mradi huu unahusisha uandaaji wa michoro, ujenzi wa matenki, ununuzi na ufungaji wa pampu kubwa za kusukuma maji; uagizaji na ulazaji wa mabomba makubwa ya ugawaji maji na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji mitaani.

Maeneo yatakayonufaika na mradi huu anasema ni pamoja na Salasala, Goba, Bunju, Wazo, Makongo, Changanyikeni, Bagamoyo na ukanda maalumu wa EPZA ambayo kimsingi yanahudumiwa na mtambo wa Ruvu Chini. Eneo jingine litakalonufaika na mradi kwa mujibu wa Mdaku ni lile lililopo kati ya Mbezi Luis na Kiluvya, mkoani Pwani ambalo huhudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu. Hivyo kutokana na baadhi ya maeneo ya mradi huu kuwa katika miinuko, matangi mapya yatajengwa sehemu za miinuko na pampu maalumu zilizo na nguvu zitafungwa ili kuweza kusukuma maji hadi katika maeneo ya miinuko, ma matanki, anasema.

“Ili kuhakikisha kuwa pampu hizo zinapata umeme wa kutosha na zinafanya kazi kwa uwezo unaokusudiwa, Dawasa imekuwa ikifanya mawasilano ya karibu na Shirika la Umeme (Tanesco) ili kwa upande wao, waweze kuhakikisha kuwa umeme wa kutosha unapatikana,” anasema. Mdaku anasema mradi huu unaotekelezwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Dawasa, unajengwa na kampuni kutoka nchini India ya Jain Irrigation chini ya usimamizi wa kampuni ya ushauri ya WAPCOS kwa gharama ya Dola za Marekani 32,927,222.45. Mdaku anatoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili kazi iweze kwenda kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa ili kutimiza ahadi ya Serikali ya kuwapatia wananchi wake huduma bora za maji.

No comments:

Post a Comment