Aidha, Mamlaka ya Hali ya Hewa ilitoa taarifa inayoonesha kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali mkoani Tanga zimefikia kiwango cha juu kisichowahi kurekodiwa tangu mwaka 1949, sawa na takribani miaka 68 iliyopita.
NYUMBA ZILIVYOKIMBIWA
Katika baadhi ya maeneo ambayo waandishi wa Nipashe walitembelea jijini Dar es Salaam jana, hasa ya mabondeni, ilionekana kuwa baadhi ya nyumba zimekimbiwa na wakazi wake na kubaki tupu baada ya kuzingirwa na maji, huku wengine wakionekana kuhamisha vitu vyao kwenda kujihifadhi katika maeneo salama.
Katika eneo la Boko Basihaya, kwenye Manispaa ya Kinondoni, nyumba takribani 20 zilishuhudiwa zikiwa tupu baada ya wakazi wake kuzihama kutokana na kujaa maji. Pia familia sita zilidaiwa kutafutiwa makazi ya kujihifadhi na serikali ya mtaa, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa mwenyekiti wa mtaa huo, Marino Sindule.
Nyumba nyingi maeneo hayo zilionekana zikiwa zimezingirwa maji hadi kwenye usawa wa madirisha.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo waliokutwa wakiwa katika harakati za kuhama na kujitambulishwa kwa jina la Raphael Lugendo aliiambia Nipashe kuwa eneo lao limefurika maji kutokana na miundombinu kutoyaruhusu yapite.
Alisema kuwa hivi sasa imemlazimu kuhama kwa kuwa nyumba anayoishi imefurika maji.
“Hata sasa hapa nilipo maji yanaingia muda siyo mrefu… nitajibana dukani (kwa jirani) maana hata haya maji siyo salama. Choo chenyewe kinaelea kwenye maji kama unavyoona,” alisema Lugendo.
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mussa Mwinyimkuu alisema wanataabika kwa sababu nyumba aliyopanga imefurika maji na hivyo amelazimika kuomba msaada wa kuhifadhi baadhi ya vyombo vyake kwa majirani walio katika eneo la juu lisilokumbwa na balaa hilo.
“Hi mvua imezidi sana, sijawahi kuiona,” alisema Mwinyimkuu.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Basihaya, Sindule, alisema kuwa bado wanaendelea kufanya tathmini rasmi ya athari zilizotokea, lakini hadi sasa kuna nyumba takribani 20 zilizofurika maji katika eneo lao.
Alisema serikali ya mtaa kwa kushirikiana na wananchi wametengeneza mtaro wa kupitisha maji kuelekea katika eneo la Dawasco pamoja na kuzibua maeneo yaliyokuwa yamezibwa ili maji yapite vizuri.
“Kuna nyumba zimeingia maji na sasa watu wameondoka… wamiliki waliamua kuzikimbia kutokana na tatizo hilo,” alisema.
Alisema kuna baadhi ya nyumba zilishakimbiwa kitambo na wamiliki wake na hivyo baadhi ya watu hukaa bure wakati wa kiangazi, mvua zinaponyesha nao huzikimbia na kuhamia kwingineko kusalimisha maisha yao.
“Kila ikifika wakati wa masika wanachukua vyombo vyao, wanaondoka… mvua zikiisha na maji kukauka wanarudi tena. Ni kama wamezoea mafuriko,” alisema.
Aidha, hali ya mafuriko iko hivyo pia katika maeneo mengine kadhaa ya mabondeni jijini Dar es Salaam na kuwaacha wakazi wake katika hali ngumu, wakiwamo kwenye maeneo ya bonde la Msimbazi na Mkwajuni.
Katika eneo la Afrikana, baadhi ya barabara zilionekana kufurika jana huku baadhi ya mifereji ikionekana kuziba na kuchangia kadhia ya kutuwama kwa maji.
Katika eneo la Buguruni, Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Faru, Simba Said Simba, alisema kuwa eneo lake limepata madhara pia kwa kuwa mvua zinazoendelea zimesababisha nyumba nyingi kuzingirwa na maji.
Alisema hivi sasa wanasubiri kufanya tathmini zaidi kufahamu idadi ya nyumba zilizopata madhara, lakini kwa ujumla hali ni ya kuhuzunisha kwa baadhi ya wananchi wake.
TAARIFA TMA
Mkurugenzi wa Utafiti wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang'a, alisisitiza kuwa ni vyema wananchi wakazingatia ushauri wao na kuchukua tahadhari kungali mapema kutokana na taarifa wanazotoa kuhusiana na hali ya mvua, hasa kwa wakazi waishio maeneo ya bondeni.
Akizungumzia kiwango cha mvua hizo, alisema mkoani Tanga imerekodiwa ya kiwango cha juu zaidi kuwahi kutokea kwa miaka mingi.
Alisema mvua iliyonyesha mkoani humo (Tanga) Mei 9 mwaka huu, ni ya milimita 316 ndani ya saa 24 na kiwango hicho hakijawahi kurekodiwa kwa miaka mingi.
Akizungumzia jijini Dar es Salaam, alisema bado hawajafanya tathmini, lakini kwa mwaka 2014 kulikuwa na kiwango kikubwa zaidi baada ya kunyesha mvua ya milimita 138 kwa saa 24 na kiwango cha juu kwa historia ya kituo cha Dar es Salaam ni mwaka 1953 wakati iliponyesha mvua ya kiwango cha milimita 167.4.
Alisema mvua za sasa zinatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi huu.
No comments:
Post a Comment