Friday, April 6, 2018

MAAFISA KILIMO WAKABITHIWA PIKIPIKI GEITA

Halmashauri ya Mji wa Geita imetoa pikipiki nne(4) kwa Maafisa kilimo wa Kata ili waweze kutimiza wajibu wao wa kuwatembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na wakulima katika maeneo yao.

Akikabidhi pikipiki hizo,mapema jana katika Ofisi za Halmashauri ya Mji Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Halmashauri hiyo kupitia viongozi wake kwa kuona umuhimu wa kununua pikipiki hizo ili ziweze kuwasaidia wataalam wa kilimo kutekeleza majukumu yao ya kila siku katika kutoa huduma za ugani kwa wakulima.

Mkuu wa Mkoa wa Geita amewataka Maafisa ugani waliopatiwa pikipiki hizo wafanye kazi zao kwa weledi mkubwa katika kuwafikia wakulima wengi zaidi na kutoa huduma stahiki na tahmini ya kina ifanyike juu ya ufanisi wa Maafisa ugani wote wenye vyombo vua usafiri.

Mhandisi Robert Gabriel amefafanua kuwa Mkoa wa Geita umejipanga kuanzisha kilimo cha korosho ili kuongeza mazao ya biashara, hivyo ujio wa pikipiki hizo utasaidia sana kutembea na kubaini maeneo mbalimbali yanayofaa kwa kilimo cha zao la korosho.

Mkuu wa Mkoa wa Geita ametumia fursa hiyo kuziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Geita kuiga mfano thabiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kufikisha lengo la asilimia 100 kwa kuwawezesha Maafisa Ugani wote nyenzo za usafiri ili wakasimamie shughuli za kilimo. Pia watenge asilimia 10 ya mapato yatokanayo na ushuru wa mauzo ya pamba ili fedha hizo zisaidie kutoa huduma za ugani ikiwa ni pamoja na kununua pikipiki.

Kwa upande wao Maafisa Ugani wa Kata za Bung’wangoko na Mtakuja, Ndg. Allan Kisomeko na Jackline Otieno kwa niaba ya wenzao wameishukuru Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuwapatia vyombo vya usafiri vitakavyowawezesha kufanya kazi kurahisi na kuwafikia wakulima wengi kwa muda mfupi, tofauti na awali walipokuwa wakitembea kwa miguu au kutumia usafiri wa baiskeli kuwafuata wakulia katika maeneo yao ndani ya Kata wanazozihudumia.

Halmashauri ya Mji wa Geita imetoa pikipiki nne aina ya Honda ambazo zimegharimu kiasi cha Shilingi bilioni kumi na mbili na laki nane(12,800,000/= )kufuatia agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mheshimiwa Kassimu Majaliwa alipofanya kikao na Wakuu wa Mikoa kumi inayozalisha zao la pamba nchini mwezi Septemba 2017 mjini Dodoma, ambapo aliziagiza Halmashauri zote katika Mikoa hiyo kununua pikipiki kwa ajili ya Maafisa ugani wao ili waweze kuwafikia wakulima wengi kwa muda mfupi.

No comments:

Post a Comment