Mke wa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) wa Uvinza mkoani Kigoma, Amedeus Malenge, ambaye aliuawa kikatili juzi, amesema kifo cha mume wake kina utata.
Akizungumza na Nipashe nyumbani kwake, Buguruni jijini Dar es Salaam, ambako ndiko msiba uliko, Mary Amedeus, alisema kifo hicho kimejawa utata kutokana na mazingira yaliyojitoleza kuhusiana na tukio hilo.
Akitaja sababu za kudhania kuwa kifo hicho ni cha utata, Mary alisema siku ya shughuli ya kumuaga binti yake (sendoff) Alhamis iliyopita, kulitokea mzozo wa kifedha ukumbini.
Alisema kamati ya maandalizi ya shughuli iliahidi kumpa mtoto fedha taslimu kama zawadi, lakini ilipofika muda wa kufanya hivyo ukumbini, mke mwenzake ambaye alikuwa ndiye mweka hazina wa shughuli hiyo hakuzitoa.
“Binafsi sikutaka kuingilia mzozo uliozuka," alisema kwa majonzi Mary. "Nilikaa pembeni na baadaye nikaondoka kwa hiyo sikujua kama waliumaliza vipi."
"Siku ya harusi ilipofika (Jumamosi iliyopita) huyu mwanamke hakuja na sikupata muda wa kumuuliza mume wangu waliafikianaje kuhusu zawadi ya mtoto."
Alisema mume wake alikuja Dar es Salaam kutoka Kigoma alipo kikazi kwa ajili ya shughuli ya mtoto wao na Jumapili aliondoka Buguruni bila kueleza anakoelekea.
“Baada ya muda alinitumia fedha (kwa njia ya simu) na kuniambia ninunue umeme wa Luku na nyingine za chakula... hatukuwasiliana tena hadi Jumanne nilipopigiwa simu na Kamanda (wa Polisi) ambaye alinijulisha kuwa mume wangu ameuawa.”
Alisema mume wake amejenga nyumba Kinyerezi ambako wakati mwingine anapokuja Dar es Salaam huenda kukaa huko.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, aliiambia Nipashe jana kuwa wahusika na mauji hayo ni vibaka.
Alisema vibaka hao hawakuwa na bunduki zaidi ya mapanga waliyokuwa wamebeba, ambayo waliyatumia kumshambulia nayo ofisa huyo maeneo ya kichwani.
Sirro alisema vibaka hao walimvamia na kumtaka awape fedha lakini aliwajibu hana ndipo wakaanza kumshambulia.
Alisema walimnyang’anya simu zake mbili za mkononi katika shambulizi hilo la mapanga hadi kukutwa na mauti.
“Hili tukio lilifanywa na vibaka wala hawakuwa majambazi na walimvamia na kuanza kumshambulia na mapanga kichwani lakini ni baada ya kumuomba hela na yeye hakuwa nazo, pia walichukua simu zake mbili,”alisema Kamanda Sirro.
Alisema wanawashikilia watuhumiwa kadhaa kuhusiana na tukio hilo na kwamba wanaendelea kuwasaka wengine waliohusika.
“Hatuwezi kutaja idadi yao kwa sababu upelelezi bado unaendelea wa kuwasaka wote waliohusika na tukio hilo,” alisema Kamanda Sirro.
WAMETEKA WALINZI
Ingawa Kamanda Sirro amedai Malenge aliuawa na vibaka, habari za kuaminika kutoka Kinyerezi juzi zilisema marehemu ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) ya Kibaha kabla ya kuhamishiwa Uvinza, alikutana na watu ambao walikuwa wamewateka walinzi wa nyumba yake iliyoko Kinyerezi wakati akirudi kutoka katika matembezi.
“Taarifa za awali tulizopata ni kwamba alikuwa anatoka kula maana pale anapoishi haishi na mke,” alisema mmoja wa mtu aliyewahi kufanya kazi na marehemu.
"Ndipo alipokuwa anarudi akawakuta walinzi wake wametekwa nje karibu na nyumbani kwake, akasimamisha gari na kushusha kioo na kuuliza kulikoni.
"Wakati anauliza wale watu walimvamia katika gari lake na kumpiga kichwani na kitu kizito ambapo alifariki papo hapo."
Aidha, Kamanda Sirro, alisema wanamtafuta Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kinyerezi kwa ajili ya mahojiano, aeleze kwanini kwenye mtaa wake hakuna vikundi vya ulinzi shirikishi.
Alisema alishaagiza maeneo ambako mitaa haijajengeka na hakuna watu wengi, kunatakiwa kuwa na vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuimarisha ulinzi.
“Mtaa ambako ameuliwa huyu Ofisa wetu hakuna watu wengi ni maeneo ya ndani ndani, kulitakiwa kuwe na vikundi vya ulinzi shirikishi kwa ajili ya kulinda usalama wao lakini hakuna hivyo nimemuita Mwenyekiti wa ule mtaa aje ofisini atuambie kwanini kwenye mtaa wake hakuna ulinzi shirikishi,” alisema.
No comments:
Post a Comment