Thursday, May 18, 2017

DAKTARI ALIMA BUSTANI YA VIAZI HOSPITALI KUSAIDIA UTAPIAMLO


Mbunge wa Viti Maalumu mkoani hapa (CCM) Azza Hilali, amepongeza uanzishwaji wa shamba darasa la viazi lishe katika zahanati ya kata ya Solwa, Shinyanga vijijini, ili kupambana na tatizo la utapiamlo kwa watoto kwenye kata hiyo.

Alisema uanzishwaji wa shamba darasa litakuwa chachu kwa wazazi katika kuhakikisha watoto wao hawapatwi na matatizo ya utapiamlo, ikiwa idadi kubwa ya wananchi wa mkoa huo hupenda kuona kwanza kwa vitendo ndipo watekeleze, elimu ambayo ame amini itazaa matunda.

Alitoa pongezi hizo wakati akigawa vifaa tiba katika zahanati hiyo ambayo ni vitanda viwili vya kisasa kwa ajili ya kujifungulia na viti viwili vya magurudumu vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 4.7, na kuelezwa kuwa zahanati hiyo ina lima shamba la mfano la viazi lishe ili kupambana na utapiamlo.

“Hili ni jambo ambalo linahitaji pongezi kubwa, tangu nifanye ziara zangu kwenye huduma za kiafya sijawahi kukutana na suala hili kuwa hospitali ina lima shamba la mfano la viazi lishe ili kupambana na utapiamlo kwa watoto, na waomba wazazi elimu hii muitumie ipasavyo kukomboa afya za watoto wenu,” alisema.

Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Dk. Edwin Ibrahim, alisema aliamua kuanzisha shamba hilo baada ya kuona watoto wengi wanaozaliwa kwenye kata hiyo wanakabiliwa na tatizo la utapiamlo, na alipofanya utafiti aligundua kuna ukosefu wa elimu ya lishe kwa wazazi.

Alisema kutokana na ukosefu wa elimu hiyo, ndipo akaamua kuanzisha shamba darasa la viazi hivyo kwa kushirikiana na wazazi, watakao kuwa wakivuna na kulisha watoto wao ili kupata elimu kwa vitendo, na pia watakuwa wakichukua mbegu kwenda kulima kwenye mashamba yao ili kutokomeza tatizo hilo.
Nao baadhi ya wazazi hao Grace Richard na Debora Samweli, waliahidi kuzingatia elimu hiyo hasa maeneo ya vijijini.

No comments:

Post a Comment