Monday, May 8, 2017

ALIYEFUFUKA RUKWA ADAIWA RAMBIRAMBI

MFUGAJI mmoja wilayani Kalambo katika mkoa wa Rukwa amegoma kumrejesha kwa ndugu zake kijana ambaye iliaminika amekufa kwa kuliwa na fisi, lakini akakutwa akichunga mifugo; akidai kwanza malipo ya sh. milioni moja alizotoa kwenye msiba wake.Tukio hilo la kushangaza lilitokea mwishoni mwa wiki baada ya kijana huyo kukutwa akichunga ng'ombe wa Juma Maeka, ambaye aligoma kumrejesha kwa ndugu zake akitaka kwanza kulipwa sh. milioni moja.Mkazi wa kijiji cha Tunyi kata ya Mabwekoswe wilayani Kalambo mkoani Lukwa, Mtipa Sisunzu (20) alipotea Septemba, mwaka jana katika mazingira ya kutatanisha na ndugu zake waliweka msiba wakiamini alikufa kwa kuliwa na fisi.Lakini Sisunzu alizua taharuki kijijini hapo wiki iliyopita baada ya kukutwa akichunga ng'ombe wa Maeka, hali iliyopelekea ndugu kushikwa na butwaa.Diwani wa kata hiyo, Julias Siwale alisema kabla ya kupotea, kijana huyo alikuwa akifanya kazi ya kuchunga ng’ombe wa mfugaji huyo.Baada ya kupotea kwake na kuwapo kwa msiba nyumbani kwao, alisema Siwale, Maeka alitoa sh. milioni moja kwa ajili ya kusaidia msibani.Alisema baada ya msiba kumalizika, kila mtu aliamini kuwa kijana huyo alikuwa amefariki dunia.Lakini wanakijiji walikuja kushangaa baada ya ndugu wa kijana huyo kumkuta akichunga ng’ombe wa mfugaji huyo katika moja ya mbuga zilizopo mbali na kijiji hicho.Alisema baada ya kumtaka warudi nae nyumbani, Maeka aliwakatalia akitaka kulipwa fedha ambazo alitoa wakati wa msiba na kupelekea kujitokeza kwa malumbano baina yao.Diwani Siwale alisema baada ya malumbano kuwa makubwa, ikawalazimu kama uongozi wa kata kuingilia kati na kumwamuru mfugaji huyo kumrejesha kijana huyo kwa ndugu zake sambamba na kumpiga faini ya sh. 100,000 kama fidia usumbufu aliowapa ndugu wa kijana huyo.Mtendaji wa kata hiyo, Oswald Kalindo alisema awali kila mtu aliamini kijana huyo alikuwa amefariki dunia kwa kuliwa na fisi kwani walimtafuta kila kona ya kijiji na maeneo mengine kwa muda mrefu bila mafanikio.Alisema kupatikana kwa kijana huyo kumeleta faraja kwa wakazi wa kata hiyo kutokana na kwamba kila mmoja alikuwa na shaka juu ya kupotea kwake.Alisema wanajipanga kuitisha mkutano kuzungumzia suala hilo."Wananchi wametuomba viongozi tuitishe mkutano mkuu ili waweze kuzungumzia hali hii wakidai huenda kuna vijana wengi waliodaiwa kufa wakawa hai wakifanyishwa kazi za kuchunga ng'ombe au kulima mashamba," alisema Kalindu.

No comments:

Post a Comment