Monday, April 24, 2017

Yanga: TFF Wanatunyima Ubingwa


KOCHA Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, amelitupia lawama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na kitendo cha kupangiwa wiki mbili pekee kumaliza mechi zao zilizobaki.

Yanga inatetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 56, nyuma ya vinara Simba wanaoongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 62.

Mei 6 Yanga itacheza na Tanzania Prisons, Kagera Sugar (Mei 9), Mbeya City (Mei 13), Toto Afrika (Mei 16), kabla ya kwenda Mwanza kucheza mchezo wa mwisho dhidi ya Mbao utakaopigwa Mei 20, mwaka huu.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwambusi alisema kuwa kitendo cha mechi zao zilizobaki kupangwa ndani ya muda mfupi ni kama kuwaondoa kwenye mbio za ubingwa msimu huu licha ya kuwa wametengeneza viporo kutokana na kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa.

“Kiukweli hapo hatuna la kuzungumza kwa sababu wanaopanga ratiba ni TFF, hakuna asiyetambua kwamba tulikuwa tunawakilisha nchi katika michuano ya kimataifa halafu ratiba ya mashindano ya Caf hatukuitengeneza sisi na ilikuwa lazima timu iwakilishe.

“Sasa utakuta mechi zote zimepangwa karibu yaani sawa na wiki mbili, zinaumiza wachezaji na zinatupa sisi kila wakati kujiandaa kwa sababu ukiisha mchezo mmoja kunakuwa na mwingine, hivyo inasababisha wachezaji kuwa na uchovu kutokana na kukosa muda wa kupumzika ila sasa tutafanyaje kwa kuwa ni mpangilio wa chama chetu za soka? Tutacheza ili kumaliza,” alisema Mwambusi.

No comments:

Post a Comment