Monday, April 24, 2017

Mmarekani aliyekamatwa Korea Kaskazini atambuliwa

Bw Kim amekuwa akifunza katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Pyongyang (PUST)

Chuo kikuu kimoja nchini Korea Kaskazini kimesema raia wa Marekani aliyekamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa nchi hiyo Jumamosi alikuwa mhadhiri katika chuo hicho.

Wamesema jina lake ni Kim Sang-duk, lakini pia amekuwa akifahamika kamaTony Kim.

Mhadhiri huyo ambaye ni Mmarekani wa asili ya Korea amekuwa akifunza katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Pyongyang (PUST) kwa wiki kadha kabla ya kukamatwa kwake.

Chuo kikuu hicho hata hivyo kimesema masuala yaliyopelekea kukamatwa kwa Bw Kim hayana uhusiano wowote na chuo hicho.

Bw Kim alikamatwa alipokuwa anajiandaa kuondoka Pyongyang.

Maafisa wa Korea Kaskazini bado hawajasema sababu iliyochangia kukamatwa kwake.

Shirika la habari la Korea Kusini Yonhap limesema Bw Kim, ambaye umri wake ni miaka hamsini hivi, alikuwa anashiriki katika mipango ya kutoa misaada na alikuwa Korea Kaskazini kufanya mashauriano kuhusu juhudi za kusaidia watu wasiojiweza.

Shirika hilo limesema Bw Kim aliwahi kuwa profesa katika chuo kikuu cha Yanbian nchini China.

Chansela wa chuo kikuu cha PUST, Park Chan-mo, amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema Bw Kim "alikuwa anajihusisha na shughuli nyingine nje ya PUST kama vile kusaidia kituo cha mayatima."

Raia wa tatu wa Marekani kuzuiliwa

Bw Kim amezuiliwa kipindi ambacho wasiwasi umekuwa ukiongezeka katika rasi ya Korea huku meli za kivita za Marekani zikielekea eneo hilo.

Korea Kaskazini imetishia kuzishambulia meli hizo.

Marekani kwa muda imekuwa ikiituhumu Korea Kaskazini kwa kuwakamata na kuwazilia raia wake kisha kuwatumia kama rehani.

Bw Kim sasa ni raia wa tatu Mmarekani kuzuiliwa na Korea Kaskazini.

Mwezi Aprili mwaka jana, Kim Dong-chul, 62, raia wa Marekani aliyezaliwa Korea Kusini, alihukumiwa kifungo cha miaka 10 na kazi ngumu baada ya kupatikana na makosa ya kufanya ujasusi nchini humo.

Alikuwa amekamatwa Oktoba mwaka uliotanguliwa.

Mwanafunzi Mmarekani Otto Warmbier, 21, naye alikamatwa Januari mwaka jana akijaribu kuiba bango la propaganda hotelini alipokuwa ziarani Korea Kaskazini.

Alihukumiwa kufungwa jela miaka 15 na kazi ngumu kwa makosa ya uhalifu dhidi ya dola Machi mwaka 2016.

No comments:

Post a Comment