Tuesday, April 25, 2017

SIMBA ,YANGA MAFICHONI FA

MENEJA WA SIMBA, MUSSA HASSAN 'MGOSI'.

,KATIKA kuhakikisha zinaimarisha vikosi vyao mapema kuelekea mechi za hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA, Simba iliondoka jijini jana kuelekea Morogoro ilipopata makali ya Ligi Kuu Bara, wakati Yanga pia ilianza safari ya kuifuata Mbao FC mapema jijini Mwanza.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Simba, Mussa Hassan 'Mgosi' alisema wameamua kwenda kujifua Morogoro kwa sababu ni mkoa ambao umewasaidia kuvuna pointi nyingi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Mgosi alisema mechi dhidi ya Azam FC itakayopigwa Jumapili ni zaidi ya fainali kwa sababu ni daraja la kuelekea nafasi moja ya kushiriki mashindano ya kimataifa hapo mwakani.

"Tunaondoka jioni ya leo (jana) kwenda Morogoro, tunaamini ni mahali salama na lengo letu ni kuongeza nguvu zilizopungua, mechi yetu ni ngumu na hasa ukizingatia Azam wameshatoka kwenye mbio za ubingwa wa Bara, hatutaki kurejea makosa," alisema Mgosi.

Aliongeza kuwa wanafurahi kuona beki Method Mwanjali aliyekuwa majeruhi anaweza kucheza mchezo huo endapo Kocha Joseph Omog ataamua kumpanga.

Naye Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, aliliambia gazeti hili kuwa lengo la kwenda Mwanza mapema ni kutaka wachezaji wao wazoee uwanja na pia wanafahamu uzuri wa Mbao.

"Timu ikifika hatua ya nusu fainali ujue si mbovu, tutaingia kwa mbinu na mikakati ya kusaka ushindi bila kusema hawa ni wageni kwenye ligi, nao walipambana hadi wamefika hatua hii, tunataka kutetea ubingwa wetu," alisema meneja huyo.

Aliongeza kuwa watakapofanikiwa kutinga hatua ya fainali, tayari watakuwa wamejiweka mguu mmoja ndani kwenye kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa hapo mwakani.

Yanga ikiwa na Mholanzi Hans van der Pluijm mwaka jana ilishinda kombe hilo baada ya kuwafunga Azam FC katika mechi ya fainali huku pia ikiwa imeshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment