Friday, April 21, 2017

SAFARI YA SAMATTA ULAYA YAISHIA ROBO FAINALI


SAFARI ya Nahodha wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta katika michuano ya Ulaya imefikia tamati hatua ya Robo Fainali katika msimu wake wa kwanza kabisa.
 
Hiyo inafuatia klabu yake, KRC Genk kutolewa na Celta Vigo ya Hispania baada ya sare ya 1-1 usiku wa Alhamisi Uwanja wa Luminus Arena katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali.
 
Matokeo hayo yanamaanisha Genk inatolewa kwa jumla ya mabao 4-3 baada ya kufungwa 3-2 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Hispania.
 
Katika mchezo wa leo, mabao yote yalifungwa na makinda wa miaka 22, kiungo Mdenmark mwenye asili ya Uganda, Pione Sisto Ifolo Emirmija akianza kuifungia Celta Vigo dakika ya 63, kabla ya mshambuliaji Mbelgiji, Leandro Trossard kuisawazishia Genk dakika ya 67.   
Mbwana Samatta wa (pili kushoto) akipambana katikati ya wachezaji wa Celta Vigo kwenye mchezo huo  
Ikumbukwe, Pione Sisto alifunga bao la kwanza katika ushindi wa 3-2 wa Celta Vigo kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Balaidos, Vigo.
 
Mchezo huo ulikuwa wa 52 kwa Samatta tangu ajiunge na Genk Januari mwaka jana akitokea TP Mazembe ya DRC akiwa amefunga mabao 18.
 
Kati ya mechi hizo 52, michezo 18 Samatta alicheza msimu uliopita na 33 msimu huu na kati ya hiyo, ni michezo 32 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na 22 msimu huu.
 
Mechi 19 kati ya hizo alitokea benchi, nane msimu uliopita na 11 msimu huu, wakati 11 hakumaliza baada ya kutolewa, tano msimu uliopita na sita msimu huu na katika mabao hayo 18, 12 amefunga msimu huu na sita msimu uliopita.
 
Kikosi cha KRC Genk kilikuwa: Ryan, Uronen, Colley, Brabec, Castagne, Berge, Malinovskyi (71 'Writers), Pozuelo, Trossard, Buffalo/Boetius dk71 na Samatta.
 
Celta de Vigo: Alvarez, Jonny, Cabral, Fontas, Mallo, Radoja, Hernandez, Sisto, Wass/Jozabed dk79 Aspas na Guidetti/Beauvue dk41/Roncaglia dk91.

No comments:

Post a Comment