Friday, April 21, 2017

PM AKATAA WAINGEREZA KUITWA KUMSAKA SAANANE



WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekataa kuitwa kwa kikosi cha upelelezi cha Polisi wa Uingereza kuja kuchunguza tukio la kupotea kwa Ben Sanane ambaye ni msaidizi wa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe

.Waziri Mkuu Majaliwa alitoa msimamo huo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.
Mbowe aliitaka serikali kuomba msaada wa Scotland Yard kuchunguza kupotea kwa Sanane.

Mbali na tukio hilo, Mbowe alitaka taasisi hiyo pia ichunguze matukio ya utekaji watu na kuuawa kwa askari polisi mara kwa mara katika mkoa wa Pwani.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz aliiambia Nipashe mwezi mmoja uliopita kuwa ofisi yake haikuwa imefanikiwa kupata taarifa za kilichompata Saanane.

Sanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba mwaka jana.

Majaliwa alisema serikali haiwezi kualika kikosi hicho cha polisi wa malkia wa Uingereza kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini vina uwezo mkubwa wa kuchunguza matukio ya uhalifu yanayotokea.

Aidha, Majaliwa alisema matukio ya utekaji na mauaji ya polisi yaliyotokea vyombo vya ulinzi na usalama bado vinaendelea na uchunguzi na pindi utakapokamilika taarifa itatolewa.

Mbowe alisema ni miezi sita sasa imepita tangu kupotea kwa msaidizi wake huyo na hakuna taarifa yoyote ya serikali kuhusu tukio hilo.

Alisema hivi sasa taifa lina hofu, Watanzania wana hofu ya kikatiba na pia watu wanapotea ovyo hali inayosababisha hofu zaidi kwa Watanzania.

Mbowe alisema Serikali inapaswa kuomba msaada wa kiuchunguzi kama ilivyowahi kufanywa na Kenya alipouawa kiongozi wa juu wa serikali, Robert Auko, katika mazingira ya kutatanisha. Alisema waliomba msaada katika taasisi hiyo ya Uingereza kuja kuchunguza.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali ina mahusiano mazuri na mataifa kadhaa ambayo wanashirikiana katika masuala ya ulinzi.

Alisema matukio yanayotokea nchini kwa sasa vyombo vya ulinzi na usalama bado vina uwezo wa kufanya uchunguzi na kutambua wahusika wa matukio hayo, na kwamba kwa sasa vyombo hivyo bado vipo katika uchunguzi.

“Kuhusu matukio yanayotokea hapa nchini, nikuhakikishie (Mheshimiwa Mbowe) vyombo vyetu vinauwezo wa kufanya ufuatiliaji wa kutambua matukio ya awali ya mtu kufariki au kutoweka mahali baada ya familia kutoa taarifa na uchunguzi ukafanyika," alisema Majaliwa.

“Lazima mtuamini kuwa serikali ina uwezo wa kutambua vyanzo na kudhibiti matukio yanayotokea nchini.

"Serikali haina kikomo cha uchunguzi kutegemeana na uhalisia wa tukio lenyewe, kuhusu suala la Ben Sanane uchunguzi ukikamilika taarifa itatolewa.”

Majaliwa alisema Serikali inatambua kuwapo na matukio yanayotokea nchini na kwamba matukio hayo yameachwa kwa vyombo vya usalama kufanyiwa kazi.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema Watanzania waipe muda serikali kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya kazi ya kuchunguza ili kuweza kubaini ni nini haswa kinatokea na nani anasababisha.

POLISI KIMATAIFA
Hata hivyo, DCI Kamishna Boaz aliiambia Nipashe Machi 15 kuwa ofisi yake imetoa taarifa kwa kutumia mfumo wa kiuchunguzi kwa Jeshi la Polisi la Kimataifa (Interpol) kumsaka mwanachama huyo wa Chadema lakini bado halijapata mrejesho wowote.

Kamishna Boaz alisema licha ya taarifa nyingi walizozipata kutoka kwa watu mbalimbali juu ya kupotea kwa mwanachama huyo wa Chadema, hakuna hata moja iliyotoa mwanga wa kupatikana kwake.

Alisema wameshawahoji watu wote ambao kwa namna moja ama nyingine walionekana kuwa karibu na Sanane.

Kamishna Boaz alisema wamewahoji pia watu wote waliokuwa wanazungumzia suala hilo katika vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali, lakini hakuna mafanikio yoyote.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho cha siasa, Tundu Lissu, Saanane aliwasiliana kwa mara ya mwisho na Mbowe Novemba 14, mwaka jana na tangu siku hiyo, hawajawahi kupata mawasiliano yake ya simu na hajulikani aliko.

No comments:

Post a Comment